Rex Tillerson yupo ziarani nchini India | Matukio ya Kisiasa | DW | 25.10.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Rex Tillerson yupo ziarani nchini India

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Rex Tillerson yupo ziarani India kukutana na viongozi wa nchi hiyo juu ya masuala tofauti ikiwemo ushirikiano zaidi wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili.

Ajenda ya mkutano katika ziara ya Waziri Tillerson  nchini India ni ushawishi wa China, mustakbali wa Afghanistan na jukumu la India katika nchi hiyo iliyokumbwa na machafuko pamoja na kuimarisha uhusiano kati ya Marekani na India. Baada ya kukutana na Waziri Tillerson, waziri wa mambo ya nchi za nje wa India Sushma Swaraj ameeleza kuwa nchi hiyo imekubali kufanya mazungumzo juu ya Afghanistan huku akisema kwa pamoja India na Marekani wamejadili namna ya kuongeza ushirikiano wao wa kiuchumi.

Katika mkutano na vyombo vya habari mjini New Delhi, waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Rex Tillerson aliizungumzia Pakistan kwa kusema nchi yake ina wasiwasi juu ya udhabiti na usalama wa serikali ya nchi hiyo akimaanisha uwepo wa mashirika ya kigaidi Pakistan pamoja na ushawishi wao. Amesema mazungumzo ya namna ya kupambana na ugaidi nchini Pakistan ni mambo muhimu yaliyopo katika ajenda yao.

Kando na hayo Waziri Swaraj pia alimuambia Tillerson kuwa India ingelipenda kuendelea kuhifadhi ubalozi wake mdogo uliyopo Korea Kaskazini licha ya juhudi za Marekani za kuitaka kuitenga Pyongyang kutokana na majaribio yake ya makombora. 

Amesema India inaamini hatua za kidplomasia zinapaswa kuchukulia kushughulikia suala la Korea Kaskazini ili kuacha wazi mlango wa mawasiliano.  India na Korea Kaskazini wameendelea kuwa na ofisi za kidiplomasia katika miji mikuu ya nchi hizo lakini India hivi karibuni ilipiga marufuku uwepo wa baadhi ya ofisi.

Tillerson aliyewasili India hapo jana  baada ya kutokea Pakistan, atakutana pia na Waziri mkuu wa India Narendra Modi katika ziara yake hiyo ya siku mbili.  Kabla ya kuwasili India alikuwepo Iraq Afghanistan Qatar pamoja na Saudi Arabia.

Mwandishi:Amina Abubakar/AP/Reuters/dpa

Mahriri: Gakuba, Daniel

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com