1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Xi Jinping: Muungano wa China na Taiwan ni lazima

Daniel Gakuba
2 Januari 2019

Rais wa China Xi Jinping amesema muungano kati ya China na Taiwan hauepukiki na ndoto za uhuru wa kisiwa hicho chenye mamlaka ya ndani ni ndoto ya mchana. Amesema China haitasita kutumia nguvu ikibidi, kuhusiana na hilo.

https://p.dw.com/p/3AsXZ
China Peking Kommunistischer Parteitag Xi Jinping
Rais Xi Jinping wa ChinaPicha: Reuters/A. Song

Rais Xi ameitoa kauli hiyo katika hotuba yake katika hafla ya kuadhimisha miaka 40 tangu kutolewa kwa tamko muhimu juu ya sera ya China kuhusu Taiwan, iliyofanyika kwenye ukumbi maarufu wa umma wa China mjini Beijing leo (Jumatano).

''Tuko radhi kuweka upeo mpana kwa ajili ya muungano kwa njia ya amani, lakini kamwe hatutaruhusu aina yoyote ya harakati za kuwania uhuru wa Taiwan.'' amesema Xi na kushangiliwa na wajumbe katika ukumbe huo.

China na kisiwa cha Taiwan kilichoko umbali wa kilomita 160 kutoka China Bara, zilitengana wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1949, pale upande wa wapiganaji wa kizalendo ulioshindwa na kuunda serikali yake kisiwani humo.

Karte China Taiwan
Kisiwa cha Taiwan kilijitenga na China Bara baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1949Picha: DW

Xi amependekeza kufanyika mazungumzo ya pande mbili, ya kuweka mpangilio wa kuzileta pamoja sehemu hizo mbili kwa njia ya amani, akisema watu wa pande zote wanataka kuona zikiungana na kuwa China moja.

Nchi moja-mifumo miwili

Amesema muungano huo unaweza kuwa wa mtindo wa 'nchi moja-mifumo miwili' ambao utaheshimu muundo wa kijamii wa Taiwan na mtindo wa maisha wa watu wa kisiwa hicho, wenye kuhakikisha haki na uhuru wao wa kidini, umilikaji wa mali na haki nyinginezo.

Hata hivyo, Xi amesema ikiwa njia ya amani haitawezekana, hatoi ahadi yoyote ya China kujizuia kutumia nguvu za kijeshi kufanikisha muungano huo, akisisitiza kuwa nchi yake inayo haki ya kuchukua hatutua zozote zinazohitajika kuhusiana na suala hilo.

Watu wote wanapaswa ''kuelewa kwamba jaribio lolote la kutangaza uhuru wa Taiwan litaleta janga kubwa kwa watu wa Taiwan,'' amesema Rais Xi Jinping.

Mitazamo inayokinzana

USA Houston - Taiwans Präsidentin Tsia Ing-Wen besucht die NASA
Rais Tsia Ing-wen wa Taiwan anasema nchi yake inataka kuendelea kuwa na mamlaka ya ndaniPicha: Taiwan Presidential Office

Haijulikani madai ya kiongozi huyo kwamba watu wa pande zote mbili wanayo kiu ya kuungana tena  imepokelewa vipi kisiwani Taiwan.

Ni jana tu (Jumanne) ambapo rais wa Taiwan Tsia Ing-wen alipotamka bayana, kwamba watu wa kisiwa hicho wanaazimia kuendeleza utawala na uhuru wao wa ndani.

Ingawa kwa wakati huu China na Taiwan zina uhusiano mzuri kibiashara na kitamaduni, Taiwan inayojivunia mfumo wake wa kidemokrasia, haionyeshi shauku ya kujiunga na China iliyo chini ya utawala wa chama kimoja.

Katika hotuba yake Rais Xi Jinping amesisitiza kuwa mzozo wa Taiwan ni suala la ndani la China, na kusema mgogoro huo ambao umekuwepo kwa miaka 70 unapaswa kupatiwa ufumbuzi wa haraka, badala ya kuukabidhi kwa vizazi vya baadaye.

Mwandishi: Daniel Gakuba/ape, afpe

Mhariri: Grace Kabogo