1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Xi aahidi ushirikiano imara na Afrika

John Juma
22 Julai 2018

Rais wa China Xi Jinping akiwa ziarani Senegal amesaini mikataba kadhaa ya kibiashara

https://p.dw.com/p/31sJB
Senegal Xi Jinping auf Staatsbesuch
Picha: Reuters/M. McAllister

Rais Xi ametia saini mikataba kadhaa ya kibiashara katika ziara yake nchini Senegal, huku akiwa rais wa kwanza wa China kuwahi kuzuru Senegal kwa takriban mwongo mmoja.

Rais Macky Sall wa Senegal alimkaribisha Xi mjini Dakar kwa mazungumzo ya jioni siku ya Jumamosi (Julai 21). Japo taarifa zaidi kuhusu mikataba aliyosaini hazikubainika moja kwa moja, Sall aliwaambia waandishi wa habari kuwa yeye na Xi walizungumzia ushirikiano kati ya nchi hizo mbili, ushirikiano wa China na nchi za Afrika, na masuala ya kimataifa, huku akiisifia China kuwa miongoni mwa nchi zenye uchumi mkubwa kwa sasa ulimwenguni.

Kwa upande wake, Rais Xi aliahidi kuimarisha ushirikiano kiuchumi na bara la Afrika ambalo tayari China imezipa nchi zake kadhaa mikopo kwa ubadilishanaji wa madini na miradi mikubwa ya ujenzi wa miundombinu.

Rais wa China Xi Jinping akikagua gwaride la heshima nchini Senegal
Rais wa China Xi Jinping akikagua gwaride la heshima nchini SenegalPicha: Reuters/M. McAllister

"Kila ninapozuru Afrika, ninaona mambo mbalimbali ya bara hili na matarajio ya maendeleo ya watu wake." Xi aliwaambia waandishi wa habari, akiongeza kuwa ana imani kuhusu mustakabali wa uhusiano kati ya China na Afrika.

Xi aliwasili Senegal siku ya Jumamosi kwa ziara ya siku mbili, alikolakiwa na mamia ya watu waliobeba vijibendera vya China na Senegal, huku wakivalia mashati yenye michoro ya Xi na Sall. Senegal ni awamu ya kwanza ya ziara yake barani Afrika, ambapo siku ya Jumapili alitazamiwa kulekea Rwanda na kisha Afrika Kusini kuhudhuria mkutano wa kilele wa nchi zinazokuwa kwa kasi kiuchumi ambazo ni Brazil, Urusi, India, China na Afrika Kusini (BRICS).

Kwa sasa China inafanya biashara nyingi na Afrika kuliko nchi yoyote duniani, na hatua yake ya mara kwa mara kukurubiana na Afrika, inatofautiana pakubwa na Marekani ambayo rais wake, Donald Trump, ameonesha kiwango kidogo cha kuwa na haja nalo.

Afrika yajilimbikizia madeni kutoka China?

Baadhi ya raia wa Senegal wakipeperusha bendera za China na Senegal kumkaribisha Rais Xi wa China
Baadhi ya raia wa Senegal wakipeperusha bendera za China na Senegal kumkaribisha Rais Xi wa ChinaPicha: Getty Images/AFP/Seyllou

Miradi mbalimbali ya miundombinu inaendelezwa barani Afrika hivi sasa kutokana na mikopo inayotolewa kirahisi na China. Mikopo ambayo pia imesaidia sehemu ya mradi wa Xi wa ujenzi wa miundombinu ya usafiri unaolenga kuunganisha China kwa njia ya barabara na kusini mashariki ya China, Asia ya Kati, Mashariki ya Kati, Ulaya na Afrika kwa njia ya bahari.

China imeahidi kutoa dola bilioni 126 kutekeleza mradi huo ambao umesifiwa na wanaouunga mkono kama chanzo cha ufadhili muhimu kwa maendeleo ya nchi zinazoinukia kiuchumi.

Nchini Senegal mikopo kutoka China imefadhili ujenzi wa barabara inayounganisha mji mkuu Dakar na Touba ambao ni mji wake mkuu wa pili kwa ukubwa, na pia sehemu ya viwanda katika rasi ya Dakar.

Balozi wa China nchini Senegal alinukuliwa na vyombo vya habari mnamo mwezi Machi akisema China iliwekeza kiasi cha dola milioni 100 nchini Senegal mwaka 2017.

Mwandishi: John Juma/RTRE/AFPE

Mhariri: Mohammed Khelef