Rais wa Nigeria aahidi kuwaokoa wasichana waliotekwa nyara | Matukio ya Afrika | DW | 08.05.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Rais wa Nigeria aahidi kuwaokoa wasichana waliotekwa nyara

Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan ameahidi kuwakomboa zaidi ya wasichana 200 waliotekwa nyara na Boko Haram huku suala hilo likigubika mkutano wa dunia wa kiuchumi unaopaswa kuangazia fursa za uwekezaji barani Afrika

Akizungumza katika mkutano wa dunia wa kiuchumi kuhusu bara la Afrika WEF unaofanyika mjini Abuja Nigeria,Rais Jonathan amezishukuru nchi za kigeni zikiwemo Marekani,Uingereza,Ufaransa na China kwa kujitolea kuisadia nchi yake katika juhudi za kuwatafuta wasichana hao waliotekwa nyara kutoka shule moja ya upili tarehe 14 mwezi uliopita na Boko Haram.

Rais huyo wa Nigeria amewashukuru wajumbe waliohudhuria mkutano huo wa kiuchumi licha ya hatari iliyopo nchini humo kutokana na vitisho vya kundi hilo la Boko Haram na kukiri kuwa taifa hilo linakabiliwa na tatizo la mashambulizi ya kigaidi.

Serikali haijui waliko wasichana

Jonathan amekiri katika kituo cha kitaifa cha televisheni wiki hii kuwa hana ufahamu kuhusu mahala walipo wasichana hao.Kutekwa nyara kwa wanafunzi hao kumefunika kwa kiasi kikubwa mkutano huo muhimu wa kiuchumi unaowaleta pamoja wajumbe takriban elfu moja kutoka nchi sabini.

Raia wakiandamana mjini Abuja kutaka serikali kuwaokoa wasichana waliotekwa nyara

Raia wakiandamana mjini Abuja kutaka serikali kuwaokoa wasichana waliotekwa nyara

Ufaransa ndiyo nchi ya hivi karibuni kujitolea kuisadia Nigeria kwa kutangaza kuwa itaimarisha ushirikiano na Nigeria katika masuala ya kijasusi na kutuma maafisa wa usalama kukabiliana na Boko Haram.

Hayo yanakuja huku Boko Haram ikidaiwa kufanya mashambulizi mengine wiki hii katika mji wa Gamboru Ngala ambapo inahofiwa kiasi ya watu mia tatu wameuawa.

Kiongozi wa Boko Haram Abubakar Shekau ametishia kuwauza wasichana hao kama watumwa,hatua ambayo imelaaniwa vikali na Umoja wa Mataifa na kuonya kuwa kufanya hivyo kutapelekea waasi hao kufunguliwa mashitaka ya uhalifu dhidi ya binadamu.

Vitendo vya Boko Haram haviambatani na mafunzo ya uislamu

Wasomi wa kidini wa Jumuiya kubwa zaidi ya ushirikiano wa nchi za kiislamu OIC wamelaani vikali utekaji nyara huo na kutaka kuaachiwa mara moja.Taasisi ya kiislamu ya Fiqh ambayo ina makao yake Saudi Arabia inayoangazia mafunzo ya dini ya kiislamu imesema uhalifu unaofanywa na makundi yenye itikadi kali yanayodai kufuata mafundisho ya kiislamu yanakiuka misingi ya Quran na mafunzo ya mtume Muhammad.

Kiongozi wa Boko Haram(Katikati) Abubakar Shekau

Kiongozi wa Boko Haram(Katikati) Abubakar Shekau

Tume huru ya OIC ya kutetea haki za binadamu pia imesema leo kuwa Boko Haram imepotoka kwa kudai kuwa kuwateka nyara wasichana hao na kutaka kuwauza kunaambatana na mafunzo ya uislamu na kutaja vitendo vya kundi hilo kuwa ya kinyama.

Makao makuu ya kanisa katoliki Vatikani pia yamelaani utekaji nyara huo na kusema ni kisa cha hivi punde cha kinyama cha kundi la Boko Haram ambalo limelesababisha maafa na ghadhabu kwa watu wa Nigeria.

Mtu tajiri zaidi barani Afrika Aliko Dangote ambaye ni raia wa Nigeria ametangaza leo kuwa atawekeza kiasi cha dola bilioni 2.3 katika biashara ya sukari na mchele kaskazini mwa Nigeria akisema kubuniwa kwa nafasi za ajira katika eneo hilo ambalo ni ngome ya Boko Haram na ambayo inakabiliwa na umaskini mkubwa,ukosefu wa ajira na elimu duni kutamaliza uasi.

Wanaharakati wamekuwa wakiitaka serikali ya Nigeria kushughulikia tatizo la kutokuwepo kwa maendeleo na kusahaulika kwa eneo hilo la kaskazini mwa Nigeria ili kupunguza ushawishi wa vijana kutaka kujiunga na makundi yenye itikadi kali kama Boko Haram.

Mwandishi:Caro Robi/reuters/ap

Mhariri: Yusuf Saumu

DW inapendekeza

Matangazo

IJUE DW

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com