1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Tshisekedi kukutana na viongozi wa waasi wa Kongo

Shisia Wasilwa22 Aprili 2022

Tshisekedi ataongoza mkutano wa kwanza kati ya wawakilishi wa makundi mbali mbali ya waasi hii leo Ijumaa katika ikulu ya Nairobi nchini Kenya.

https://p.dw.com/p/4AI6h
Staatsbesuch von Präsident Uhuru Kenyatta in der Demokratischen Republik Kongo
Picha: Presidential presse office DRC

Katika mkutano wa faragha uliofanyika alhamisi na kudumu kwa zaidi ya saa saba, katika ikulu ya Nairobi viongozi wa kanda hii waliafikiana kupeleka kikosi cha kudumisha amani ili kukabiliana na ongezeko la visa vya waasi nchini humo.

Kwenye taarifa ya pamoja, marais Uhuru Kenyatta, Felix Tshisekedi, Yoweri Museveni wa Uganda na Evariste Ndayishimiye wa Burundi, pia waliafikiana kuwa makundi yote yaliyojihami yashiriki bila ya masharti kwenye mchakato wa kutatua misuguano yao na iwapo watashindwa jeshi la kikosi cha kudumisha amani cha Kanda kitaingilia kati.

Soma pia→DRC imekua rasmi mwanachama wa saba wa EAC

Uongozi wa kujitolea ?

Mkutano wa leo unajiri juma moja baada ya DRC kujumuishwa katika jumuiya ya Afrika Mashariki, Chini ya uwenyekiti wa rais Kenyatta.

"Nachukua fursa hii kumshukuru Rais Museveni, Rais Ndayishemeye, kwa kupata nafasi ya kufika hapa kushuhudia tukio hili. Kufikia hatua hii imegharimu uongozi wa kujitolea.”

Rais wa Rwanda Paul Kagame amewakilishwa kwenye mkutano huo na waziri wa mambo yya kigeni Vincent Biruta. Sababu za Rais Kagame kushindwa kufika kwenye mkutano huo zingali hazijabainika. Aidha mkutano wa Alhamisi uliafikiana kuanzisha sekreteriati ya kuhakikisha kuwa maamuzi yaliyoafikiwa yameteelezwa.

Soma pia→Mapigano yazuka baina ya jeshi la Kongo na waasi wa M23

Ni akina nani watakaoshiriki ?

Waasi wa M23 wakiwa mjini Goma mwaka 2012
Waasi wa M23 wakiwa mjini Goma mwaka 2012Picha: Simone Schlindwein

Hata hivyo msemaji wa kundi la waasi la M23 Willy Ngoma hakufichua iwapo watashiriki kwenye mkutano huo. Mazungumzo haya yanajiri chini ya mwezi mmoja baada ya DRC kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kwa muda mrefu Kigali imelaumiwa kwa kuunga mkono kundi la waasi la M23, ripoti ambazo utawala wa Kagame umekanusha. Wanajeshi wa Uganda wamekuwa Mashariki mwa DRC wakiwakabili waasi walioko katika eneo hilo.

Aidha iliafikiwa kuwa makundi yote ya kigeni yaliyojihami katika Jamhuri ya Kidemokrasia sharti yasalimishe silaha na kurejea bila masharti kwa nchi zao mbalimbali. Kwamba kukosa kufanya hivyo makundi haya yatachukuliwa kuwa adui na kukabiliwa na kanda hii kijeshi. Mkutano wa leo si wa kwanza wa kujaribu kutafuta mwarubaini, mwaka 2013 serikali ya DRC na waasi walisaini mkataba wa azimio la Nairobi wa kumaliza mzozo baina yao.

Maamuzi mengine kwenye mkutano huo yalikuwa kuvunja makundi ya waasi na kupiga marufuku fujo kama njia ya kudai haki zao siku za usoni. Rais Joseph Kabila alipongezwa na viongozi wa kanda kwa kusaini mwafaka huo. Je, mazungumzo ya leo, yatakuwa na tija? Wakati utabainisha. Kwa sasa ni kuangalia kujitolea kwa makundi hayo.