Rajoelina ajificha baada ya jaribio la mapinduzi Madagascar
14 Oktoba 2025
Rais wa Madagascar Andry Rajoelina amesema alilazimika kuondoka nchini humo na kujificha katika eneo salama baada ya kile alichokiita jaribio la kumpindua lililopangwa na wanajeshi na wanasiasa. Katika hotuba yake ya usiku wa Jumatatu, iliyorushwa kupitia televisheni ya taifa na mitandao ya kijamii, Rajoelina alikiri kuwa maisha yake yako hatarini, akisisitiza kwamba hatang'atuka madarakani.
Kwa wiki kadhaa, taifa hilo la kisiwa katika Bahari ya Hindi limekumbwa na maandamano makubwa yanayoongozwa na vijana wa kizazi cha Gen Z, waliotajwa kuwa chanzo kikuu cha wimbi jipya la upinzani. Waandamanaji wamekuwa wakilalamikia kukatikakatika kwa maji na umeme, hali ngumu ya kiuchumi, gharama kubwa za maisha na tuhuma za ufisadi serikalini.
Jumamosi iliyopita, hali ilizidi kuwa tete baada ya kikosi maalum cha jeshi, CAPSAT, kujiunga na waandamanaji na kutoa wito kwa rais pamoja na mawaziri wake kujiuzulu. Kitendo hicho kilionekana kama ishara wazi ya uasi wa kijeshi, na kikundi hicho kilidai kimechukua udhibiti wa majeshi yote ya ardhini, anga na baharini.
Rajoelina, ambaye alichaguliwa tena mwaka 2023 katika uchaguzi uliosusiwa na upinzani, alijibu kwa kusema kulikuwa na "jaribio haramu la kuchukua madaraka,” na akatangaza kuwa ameondoka nchini kwa sababu za kiusalama. Hata hivyo, hakufafanua ni wapi alipojificha.
Rajoelina asema alikataa msaada wa kijeshi kutoka mataifa ya Afrika
Katika hotuba yake, ambayo ilicheleweshwa mara kadhaa baada ya wanajeshi kuteka kituo cha matangazo ya taifa, Rajoelina alisema: "Baadhi ya marais wa Afrika walijitolea kutuma wanajeshi kuleta amani Madagascar. Nililikataa hilo, kwa sababu halilingani na maadili yetu ya Kimalagasy. Kwa sababu hiyo, nililazimika kwenda katika eneo salama kulinda maisha yangu.”
Ripoti za vyombo vya habari vya Ufaransa, ikiwemo Radio France Internationale (RFI), zinasema rais huyo mwenye uraia wa Ufaransa tangu 2014 alitolewa nchini kwa ndege ya kijeshi ya Ufaransa, chini ya makubaliano na Rais Emmanuel Macron. Hata hivyo, serikali ya Ufaransa imekataa kuthibitisha taarifa hizo, ikisema haitoi maoni kuhusu harakati za viongozi wa kigeni.
Hii ni mara ya pili kwa Rajoelina kukabiliwa na shinikizo kubwa la kisiasa tangu aliposhika madaraka kwa mara ya kwanza mwaka 2009 kufuatia mapinduzi yaliyomuondoa madarakani Rais Marc Ravalomanana. Wengi nchini humo wanasema historia inajirudia.
Mashirika ya haki za binadamu yameshutumu matumizi ya nguvu kupita kiasi kutoka kwa vyombo vya usalama katika kukabiliana na waandamanaji. Umoja wa Mataifa unasema watu angalau 22 wameuawa na kadhaa kujeruhiwa katika wiki tatu za maandamano.
Hata hivyo, Rajoelina amepinga idadi hiyo, akisema vifo vingi vilitokana na "wahalifu na waharibifu wa mali” waliopenyeza kwenye maandamano. Licha ya shutuma hizo, ametoa wito wa mazungumzo ya kitaifa na kuheshimu katiba.
Katika ujumbe wake kwa wananchi, alisema: "Wamalagasy, familia yangu, njia pekee ya kutoka katika hali hii ni kuheshimu katiba ya nchi. Tukivuka mipaka hiyo, tutazama katika umaskini mkubwa na taifa letu litapoteza mwelekeo.”
Shinikizo la waandamanaji na msimamo wa jeshi
Waandamanaji wengi sasa wanasisitiza kujiuzulu kwa Rajoelina, wakisema ameshindwa kuongoza taifa kwa uwazi na kwa maslahi ya wananchi. Mwanaharakati kijana Finaritra Andrianamelasoa alisema, "Tunataka Rais aombe radhi na kuachia madaraka. Tumepoteza ndugu na marafiki katika maandamano haya.”
Kikosi cha CAPSAT, ambacho kilimsaidia Rajoelina kuingia madarakani mwaka 2009, sasa kimegeuka kuwa tishio kwake. Kamanda wake, Kanali Michael Randrianirina, amesema jeshi limeamua kusimama upande wa wananchi, lakini amekanusha kuwa ni mapinduzi ya kijeshi, akisema hatma ya nchi iko mikononi mwa Wamalagasy.
Hadi sasa, hali ya usalama imebaki kuwa tete katika mji mkuu Antananarivo, huku magari ya kivita yakiendelea kuzunguka maeneo nyeti ya serikali na wananchi wakihimizwa kubaki majumbani. Ubalozi wa Marekani umewataka raia wake kujihifadhi, ukisema hali ni "tete na isiyotabirika.”
Wito wa Umoja wa Afrika na hatma isiyoeleweka ya Rajoelina
Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wameitaka serikali na jeshi "kurejea kwenye majukumu ya kikatiba” na kuhakikisha mgogoro unatatuliwa kwa njia ya mazungumzo.
Rajoelina amesema hatarudi nyuma. Katika ujumbe wake wa mwisho kwa wananchi, alisisitiza kuwa hatamruhusu yeyote kuivuruga Madagascar.
"Sitaiacha nchi yangu iharibiwe, na sitamruhusu yeyote kuivunja. Niko tayari kufungua milango ya maridhiano ili taifa lirudi katika utulivu.”
Chanzo: Mashirika