Rais Omar al-Bashir ziarani China | Matukio ya Kisiasa | DW | 01.09.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Rais Omar al-Bashir ziarani China

Rais wa China Xi Jinping alimkaribisha mwenzake wa Sudan, Omar Hassan al-Bashir, anayekabiliwa na mashtaka yanayohusu makosa ya uhalifu wa kivita, kama rafiki yake wakati alipowasili Beijing.

Wizara ya mambo ya kigeni ya China imesema imetoa mualiko kwa Bashiri ili ahudhurie sherehe za kuadhimisha miaka miwili ya kumalizika vita vya pili vya dunia. Bashir ni mmoja wa viongozi wa kigeni watakaohudhuria gwaride kubwa la kijeshi siku ya Alhamisi kuadhimisha miaka 70 ya Japani kusalimu amri katika vita vikuu vya pili vya dunia. Hata hivyo viongozi wakuu wa Mataifa ya Magharibi wamejitenga na sherehe hizo.

"Wewe ni rafiki wa zamani wa watu wa China, China na Sudan ni kama kaka wawili, ambao ni marafiki na washirika wa kweli. Bwana Bashiri kuja China inaonesha ushirikiano wetu ni wa nguvu," alisema rais Xi aliposalimiana na mwenzake wa Sudan aliyekuwa ameandamana na ujumbe wake. Bashir alisema amefurahi kupata mualiko wa kuhudhuria gwaride hilo la kijeshi ambapo vikosi 12,000 vitapita kati kati ya mji wa Beijing.

Bashir akabiliwa na mashtaka ICC

Watoto kwenye kambi ya wakimbizi Darfur

Watoto kwenye kambi ya wakimbizi Darfur

Aidha, wizara ya mambo ya kigeni ya China imejitetea baada ya baadhi ya ripoti kusema kumualika mtu anayekabiliwa na uhalifu wa kivita katika sherehe hizo zinazotajwa kuwa za amani ni kupingana na kile kinachosherehekewa.

Wizara hiyo imesema watu wa Afrika wakiwemo watu wa Sudan wana mchango mkubwa katika vita hivyo vya kupinga mafashisti wakitumia jina la serikali ya China katika vita vya pili vya dunia. Msemaji wa wizara hiyo Hua Chunying ameeleza nchi yake haikutia saini mkataba w aroma unaounda mahakama hiyo kwahiyo hawalazimiki kumkamata.

Mahakama hiyo ya Kimataifa ICC ilioko mjini The Hague Uholanzi, ilitoa waranti wa kukamatwa kwa Bashir mwaka wa 2009 na 2010, ikimshutumu kupanga mauaji ya kimbari na visa vengine vya kikatili Magharibi mwa Darfur. Bashir amekuwa akisafiri mara kwa mara kwa nchi jirani na Sudan lakini amejiepusha na ziara za mbali zitakazomuweka katika hatari ya kukamatwa.

Hapo Jumatatu Marekani ilielezea wasiwasi wake juu ya ziara ya Bashiri nchini China huku msemaji wa wizara ya mambo ya nje Mark Toner akisema nchi hiyo inapinga mualiko, ufadhili au usaidizi wa aina yoyote kwa mtu ambaye waranti wa kukamatwa kwawe imetolewa na mahakama ya ICC.

Mwandishi: Amina Abubakar

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com