1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiUganda

Rais Museveni wa Uganda akutana na wafanyabiashara Kampala

Lubega Emmanuel8 Mei 2024

Kinyume na matarajio Rais Yoweri Museveni angetatuwa malalamiko yao kuhusu kodi, huenda wafanyabiashara Uganda sasa wataendelea kufuata kanuni za mamlaka ya mapato kama zilivyokuwa kabla ya mgomo wao waliousitisha.

https://p.dw.com/p/4fcSL
Maduka mjini Kampala
Wafanyabiashara katika mji mkuu wa Uganda Kampala walifanya mgomo kupinga kodi kwa bidhaa za kigeniPicha: Lubega Emmanuel/DW

Hayo ndiyo yalikuwa mazingira ya mkutano kati ya Rais Museveni na wafanyabiashara ambao wiki tatu zilizopita walifanya mgomo wakipinga kodi zinazotozwa kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka mataifa ya kigeni. Rais Museveni mwanzoni alisikiliza hoja mbalimbali kutoka kwa viongozi wa wafanyabiashara hao:

Akiwajibu, Rais Museveni aliwambia kuwa wapende wasipende lazima watalipa kodi na ushuru kama ilivyopangwa na mamlaka ya mapato. Aliwambia kuwa azma ya serikali yake ni kukomesha uagizaji wa vitu ambavyo vinaweza kutengenezwa humu nchini. Ndiyo maana bidhaa hizo zikiwemo nguo, vyakula na vitu vya matumizi nyumbani vitalengwa kupandishiwa kodi. "Mnatakiwa kufahamu kuwa ikiwa mnaipenda nchi yenu mnatakiwa kuondokana na kuagiza bidhaa tunazoweza kutengeneza humu nchini. Huo ndiyo uzalendo wa kiuchumi." Alisema Museveni.

Wafanyabiashara hao aidha walikuwa wanapinga matumizi ya teknolojia kufuatilia mauzo yao na kutoa risiti za kidigitali. Hii huwezesha mamlaka ya mapato kuwatoza kodi kamili ya mauzo yao kama ilivyo katika mataifa jirani ya Kenya na Tanzania. Lakini wamefahamishwa kuwa maendeleo ya teknolojia hayawezi kuepukika katika mazingira ya sasa ya TEHAMA na biashara za kimataifa. Mfanyabiashara mmoja alsiema Teknolojia hii ni ngumu na ghali kwetu kwa sasa tunaomba iahirishwe. 

Rais Museveni alijibu kwa kusema "hatuwezi kuahirisha matumizi ya teknolojia katika kukusanya kodi na ushuru"

Lakini kwa upande mwingine, hali hii ya rais kuwa ndiye hutoa maamuzi ya mwisho kuhusu masuala ambayo wizara na taasisi zingine zingeshughulikia imeelezewa kuwa isiyostahili. Hii ni kwa sababu kiongozi wa taifa ana majukumu mengi ambayo mawaziri na watendaji wengine serikalini wanafaa kuyashughulikia.

Wafanyabiashara walimwambai rais kwamba waliamua kufanya mgomo kwa sababu mawaziri na watendaji walipuuzilia malalamiko yao kwa muda mrefu. Mchambuzi wa masuala ya kisiasa na uchumi, John Kibego, ana mtazamo huu: "Ni kama mawaziri na watu wengine hawana mamlaka ya kufanya maamuzi ni vikaragosi tu katika utawala"

Viongozi wa wafanya biashara wamesema kuwa watarudi kwenye mkutano na wenzao ili wafanye maamuzi kuhusu mwelekeo aliouchukua Rais Museveni ambaye kwa wengi wao hakutatuwa shida zao muhimu na badala yake ameziwacha kama zilivyo.