1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSenegal

Rais mpya wa Senegal kuanza na mageuzi makubwa ya kiuchumi

Hawa Bihoga
10 Aprili 2024

Rais wa Senegal Bassirou Diomaye Faye ameanza kuyatekeleza majukumu yake ya urais kwa kumuagiza waziri mkuu wake Ousmane Sonko kuandaa mpango kazi wa haraka wa kuimarisha sekta za uchumi na fedha zinazoyumba.

https://p.dw.com/p/4ebtj
Senegal Dakar 2024 | Rais wa Senegal Bassirou Diomaye Faye
Rais wa Senegal Bassirou Diomaye FayePicha: Zohra Bensemra/REUTERS

Rais Faye mwenye umri wa miaka 44 aliingia madarakani kupitia uchaguzi wa mwezi uliyopita kwa ahadi ya kufanya mageuzi makubwa, na kuwa rais mwenye umri mdogo zaidi nchini humo licha ya ukweli kwamba hakuwahi kushika wadhifa wowote wa kuchaguliwa.

Taarifa iliyotolewa hapo jana baada ya Faye kuongoza kikao chake cha kwanza cha Baraza la mawaziri, inasema rais amempa waziri mkuu wake na mshauri wa zamani Ousmane Sonko, muda wa hadi mwishoni mwa mwezi huu kuweka mpango kazi huo.

Alimuamuru Sonko kufanya mapitio jumla ya programu na mipango na kuripoti kuhusu hali jumla ya fedha za umma, ushirikiano wa kimataifa na ushirika katika taasisi za umma na binafsi.

Aliiamuru serikali kukamilisha mpango huo kufikia mwishoni mwa mwezi na kuitekeleza pasina kuchelewa pamoja na sekta binafsi ya Senegal, hii ikiwa ni sera thabiti ya kuimarisha uchumi wa taifa.

Soma pia:Rais mpya wa Senegal aagiza mpango kazi wa mageuzi makubwa ya kiuchumi

Rais Faye aliwaambia mawaziri kwamba alichaguliwa kuhakikisha taifa hilo linajitenga na mazowea ya nyuma na kutekeleza mabadiliko katika ngazi zote za maisha ya kiuchumi na kijamii nchini humo.

Changamoto za kimataifa zachangia uchumi kuzorota

Theluthi moja ya raia wa Senegal milioni 18 wanaishi katika hali ya umaskini na kiwango cha ukosefu wa ajira kiko kwenye asilimia 20.

Uchumi wake uliathiriwa pakubwa pia na janga la UVIKO-19 pamoja na vita nchini Ukraine.

Deni la taifa na mfumuko wa bei vimepanda sana huku mgogoro wa kijamii na kisiasa ulioikumba nchi hiyo katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita ukipunguza uwekezaji.

Wakati akitangaza baraza lake la mawaziri siku ya Ijumaa, Waziri Mkuu Ousmane Sonko alisema vipaumbele vya serikali vitajumlisha uundwaji wa nafasi za ajira kwa vijana, kupungua gaharama za maisha na kulinda haki za binadamu.

Tangazo la kuahirishwa uchaguzi Senegal lazusha kizaazaa

"Serikali ya matokeo ambayo naiwajibikia itajikita juu ya elimu, mafunzo, ujasiriamali na ajira kwa vijana na wanawake. Pili, kushusha gharama za maisha na kuboresha uwezo wa watu." Alisema Waziri Mkuu Sonko

"Tatu, haki, ulinzi wa haki za binadamu, utawala bora, uwazi, uwajibikaji na kuboresha demokrasia na mfumo wa uchaguzi." Aliongeza.

Soma Pia:Waziri Mkuu mpya wa Senegal atangaza Baraza la Mawaziri

Baraza la Sonko lenye mawaziri 25 na manaibu waziri watano, liliidhinishwa na Faye, aliemrithi Macky Sall, ambaye utawala wake wa miaka 12 ulishuhudia ongezeko kubwa la kutoridhika kwa umma.

Faye aliahidi mageuzi makubwa kama vile kuachana na sarafu ya pamoja ya kanda ya Afrika Magharibi ya Faranga ya CFA, ingawa alionekana kubadili msimamo huo.

Lakini wikli iliyopita inspekta huyo wa zamani wa kodi, aliahidi kufanya ukaguzi wa sekta za mafuta, gesi na madini.