1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bassirou Diomaye Faye aapishwa kuwa Rais wa Senegal

Angela Mdungu
2 Aprili 2024

Bassirou Diomaye Faye ameapishwa kuwa Rais wa Senegal. Rais huyo mwenye umri mdogo zaidi kuwahi kuiongoza Senegal ameitilia mkazo ahadi yake ya kuleta mabadiliko ya kimfumo na uhuru mkubwa:

https://p.dw.com/p/4eMY2
Bassirou Diomaye Faye ameapishwa kuwa rais mpya wa Senegal April, 2, 2024
Rais mpya wa Senegal Bassirou Diomaye FayePicha: Sylvain Cherkaoui/AP/picture alliance

Hafla ya kumuapisha rais mteule wa Senegal Bassirou Diomaye Faye, imefanyika saa chache zilizopita katika mji wa Diamniadio, karibu na mji mkuu Dakar. Faye, anakuwa rais wa awamu ya tano wa Senegal tangu taifa hilo lilipopata uhuru kutoka kwa Ufaransa mwaka 1960 .

Soma zaidi: Rais mpya wa Senegal aapishwa rasmi

Katika hotuba yake hiyo, Rais huyo ameapa kuzingatia katiba na sheria, kutetea uadilifu wa eneo na kutoacha juhudi zozote ili bara la Afrika liwe na umoja. 

Makabidhiano rasmi ya ofisi kati yake na Rais anayemaliza muda wake Macky Sall yatafanyika katika makazi ya rais mjini Dakar.

Awali baada ya kushinda uchaguzi, Faye alishatangaza vipaumbele katika uongozi wake kuwa maridhiano ya kitaifa, kupunguza gharama za maisha na kupambana na rushwa.  

Soma zaidi: Umoja wa Afrika wampongeza Faye baada ya kushinda uchaguzi wa Urais Senegal

Kiongozi huyo mpya wa Senegal  ni miongoni mwa wanasiasa wa upinzani walioachiliwa kutoka jela, sambamba na mwanasiasa maarufu wa upinzani na mwalimu wake katika siasa Ousmanne Sonko  siku 10 kabla ya uchaguzi wa Machi 24. Kuachiliwa kwake na wenzake kulitokana na msamaha uliotangazwa na Rais Sall.

Changamoto zinazomkabili Faye ni pamoja na namna ya kupata washirika bungeni 

Faye na serikali yake atakayoichagua watapaswa kuzikabili changamoto kubwa ikizingatiwa kuwa hana viti vingi bungeni. Atatakiwa kutafuta washirika ili serikali yake iweze kupitisha sheria mpya au kuitisha uchaguzi wa wabunge unaoweza kufanyika kuanzia katikati mwa mwezi Novemba.

Senegal Dakar 2024 | Hafla ya kuapishwa kwa Rais mpya wa Senegal Bassirou Diomaye Faye
Rais Bassirou Diomaye Faye akipeana mikono na mkuu wa baraza la katiba la Senegal Mamadou Badio Camar baada ya kuapishwaPicha: Zohra Bensemra/REUTERS

Moja ya changamoto kubwa zinazomkabili itakuwa kutengeneza nafasi mpya za ajira katika taifa ambalo asilimia 75 ya watu wake ni vijana wenye chini ya miaka 35 na kiwango rasmi cha ukosefu wa ajira ni asilimia 20.

Wengi wa vijana wa Senegal wamekuwa na mashaka na hatma zao kiasi cha kuhatarisha maisha yao na kujiunga na wimbi la wahamiaji wanaojaribu kufika Ulaya kinyume cha sheria.