1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Puigdemont aitwa mahakamani Madrid

Grace Kabogo
1 Novemba 2017

Mahakama Kuu ya Uhispania imemtaka aliyekuwa kiongozi wa Catalonia, Carles Puigdemont na washirika wake 13 kuwasili mahakamani wiki hii kutoa maelezo juu ya shutuma zinazomkabili.

https://p.dw.com/p/2mq3d
Pressekonferenz Puigdemont Brüssel
Picha: Reuters/Y. Herman

Ikiwa atashindwa kufanya hivyo, kiongozi huyo na serikali yake ambao kwa sasa wako mjini Brussels, wanaweza kutolewa waranti wa kukamatwa. 

Mahakama Kuu ya Uhispania jana ilimtaka Puigdemont na mawaziri wake 13 ambao utawala wao umeondolewa kufika katika mahakama ya Madrid, kutoa ushahidi wa mashtaka yanayowakabili ya uasi, uchochezi na matumizi mabaya ya fedha za umma, baada ya bunge la Catalonia wiki iliyopita kupiga kura ya kutangaza kujitenga na Uhispania kutokana na kura ya maoni iliyoleta mzozo.

Watuhumiwa hao wanatakiwa kwenda mahakamani kesho Alhamisi na Ijumaa. Lakini baada ya kwenda Ubelgiji siku ya Jumatatu baada ya mashtaka dhidi yake kutangazwa kwa mara ya kwanza, Puigdemont alisema atarejea tu nchini Uhispania iwapo atahakikishiwa kuwa kesi hiyo itasikilizwa kwa kuzingatia uhuru na haki.

Spanien - Generalstaatsanwalt José Manuel Maza hält eine Erklärung vor der Staatsanwaltschaft in Madrid
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Uhispania, Jose Manuel MazaPicha: Reuters/S. Vera

''Siko hapa kwa ajili ya kutafuta hifadhi ya kisiasa. Niko Brussels kwa sababu ni makao makuu ya Ulaya. Niko hapa kwa ajili ya kufanya majukumu yangu kwa uhuru na usalama,'' alisema Puidgemont.

Akizungumza na waandishi habari mjini Brussels, kiongozi huyo wa Catalonia amesema hawataki kukimbia wajibu wao katika mahakama na bado anataka kuendelea kupigania uhuru wa jimbo lake. Kulingana na mfumo wa kisheria wa Uhispania baada ya kesi hiyo kuanza kusikilizwa, kisha jaji ataamua iwapo Puigdemont anapaswa kwenda jela wakati akisubiri uchunguzi wa kina ufanyike.

Iwapo watapatikana na hatia, wanasiasa hao wanaweza kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 gerezani. Hapo jana, jaji wa mahakama hiyo pia alisema watuhumiwa hao wanahitaji kuwasilisha kiasi cha Euro milioni 6.2 ndani ya siku tatu kama adhabu. Kiasi hicho ni makadirio ya gharama za kura ya maoni iliyofanyikla Oktoba Mosi.

Ubelgiji yatoa taarifa

Baada ya mkutano wa jana wa Puigdemont na waandishi habari, ofisi ya Waziri Mkuu wa Ubelgiji, Charles Michel ilitoa taarifa ikisema kwamba kiongozi huyo hayuko Ubelgiji kwa mwaliko wa serikali.

Michel amesema Puigdemont ana haki na majukumu sawa kama aliyonayo raia yeyote yule wa Ulaya na kwamba serikali yake imerudia kutoa wito wa kutaka yafanyike mazungumzo ya kisiasa nchini Uhispania ili kutatua mzozo wa kisiasa nchini humo.

Brüssel PK Charles Michel Premierminister Belgien
Waziri Mkuu wa Ubelgiji, Charles MichelPicha: Reuters/F. Lenoir

Maafisa wakuu wa Umoja wa Ulaya wamekuwa wakikataa kujihusisha na mzozo huo, huku wakisema hayo ni masuala ya ndani ya Uhispania ambayo yanahitaji kutatuliwa kwa kuzingatia misingi ya katiba ya nchi hiyo.

Puigdemont ambaye anajichukulia kama rais halali wa Catalonia, amesema ataheshimu matokeo ya uchaguzi wa jimbo hilo uliopangwa kufanyika Desemba 21. Uchaguzi huo wa mapema umeitishwa na Serikali Kuu ya Uhispania, baada ya kuchukua udhibiti kamili wa jimbo hilo na kuivunja serikali ya jimbo la Catalonia kutokana na kura ya maoni ya kujitangazia uhuru.

Wakati huo huo, polisi wa Uhispania wamevamia ofisi za makao makuu ya polisi ya Catalonia, Mossos d'Esquadra yaliyoko Sabadell, Barcelona na kuchukua vifaa kadhaa vinavyohusishwa na uchaguzi wa Oktoba Mosi. Vituo vya polisi vya Girona na Tarragona pia vimevamiwa.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/DPA, AP
Mhariri: Daniel Gakuba