Puigdemont aitaka serikali Uhispania kuheshimu demokrasia | Matukio ya Kisiasa | DW | 07.04.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Puigdemont aitaka serikali Uhispania kuheshimu demokrasia

Kiongozi wa zamani wa jimbo la Katalonia Carles Puigdemont ametoa wito mpya kwa serikali kuu ya Uhispani kuanzisha majadiliano juu ya madai ya Catalonia kutaka kujitenga, baada ya kuachiliwa kutoka jela Ujerumani.

Deutschland Puigdemont - Berlin (picture-alliance/dpa/B. Pedersen)

Rais wa zamani wa jimbo la Catalonia Carles Puigdemont akizongwa na mashabiki wake mjini Berlin kabla ya kuhutubia mkutano wa waandishi wa habari, Aprili 7, 2018.

Puigdemont amewaambia waandishi habari wa Ujerumani kwamba anatarajia uamuzi wa mahakama ya Ujerumani wa kutomrejesha Uhispania kwa madai ya uasi unaonyesha kwamba majadiliano yanahitajika kuuzima mgogoro wa kisiasa unaoendelea nchini mwake.

Kiongozi huyo wa zamani wa Catalonia aliwekwa kizuizini kwa waranti wa Umoja wa Ulaya uliotolewa na serikali ya Uhispania baada ya kuingia nchini Ujerumani Machi 25. Mahakama ya jimbo la Schleswig-Holstein imeamua mashtaka ya uasi hayaruhusu kutolewa uamuzi wa mshtakiwa kurejeshwa nyumbani alipotokea.

Puigdemont alisema Uhispania inapaswa kuheshimu maazimio ya Umoja wa Mataifa kwa kuwaachia huru wafungwa wa kisiasa, akimaanisha wanasiasa kadhaa wa Catalonia wanaotaka kujitenga, waliofungwa baada ya tangazo la upande mmoja la uhuru wa Catalonia kutoka Uhispania mwaka uliopita.

Deutschland Puigdemont - Berlin (picture-alliance/dpa/B. Pedersen)

Wafuasi wa Puigedemont walimpokea kwa shangwe na vifijo kutoka jela alikokuwa anazuwia nchini Ujerumani baada ya kukamatwa.

Alisema anatumaini kurejea kuishi nchini Ubelgiji baada ya mchakato wa Ujerumani kumalizika lakini alidhamiria kubakia mjini Berlin wakati mchakato huo ukiendelea. Aliongeza kuwa atakapowasili Ubelgiji, ataendelea na shughuli zake za anazozifanya uhamishoni.

Utata wa kurejeshwa Uhispania

Maafisa nchini Ujerumani bado wanazingatia iwapo kumrejesha Puigdemont nchini Uhispania baada ya kukamatwa Machi 25 kwa waranti uliotolewa na Madrid, wakati akisafiri kupitia Ujerumani.

Serikali ya Uhispania inamtuhumu kwa "uasi" na matumizi mabaya ya fedha za umma kwa kuandaa kura haramu ya maoni kuhusu uhuru wa Catalonia mwezi Oktoba.

Siku ya Alhamisi, mahakama nchini Ujerumani iliamua kuwa hangeweza kurejeshwa kwa misingi ya uasi, kwa sababu kosa na hilo chini ya sheria ya Ujerumani, la uhaini, linahitaji mshtakiwa awe amefanya vurugu.

Puigdemont hata hivyo anaweza kurejeshwa Uhispania kukipatikana ushahidi wa madai ya kutumia vibaya fedha za umma kwa kufanya uchaguzi wa maoni wa mwaka jana uliopigwa marufuku na mahakama ya katiba ya Uhispania.

Deutschland PK Puigdemont will in Deutschland Justiz-Entscheid abwarten (picture-alliance/AA/C. Karadag)

Puigdemont akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjini Berlin siku ya Jumamosi Aprili 7, 2018 baada ya kuachiwa kutoka jela siku ya Ijumaa.

Uhispania yakataa rufaa

Waziri wa sheria wa Ujerumani Katarina Barley amesifu uamuzi huo wa mahakama, akiliambia gazeti la kila siku la Sueddeutsche Zeitung siku ya Jumamosi, kwamba uamuzi wa majaji ulikuwa "sahihi kabisa." Matamshi yake yalikosolewa mara moja kama ya "kusikitisha" na waziri wa mambo ya nje wa Uhispania, Alfonso Dastis.

"Tunahisi matamshi kuhusu uamuzi wa majaji kwa wakati huu siyo sahihi," aliwaambia waandishi wa habari katika mji wa kusini mwa Uhispania wa Seville.

Mahakama ya juu kabisa ya Uhispania inazingatia kukataa rufaa katika mahakama ya sheria ya Umoja wa Ulaya mjini Luxembourg kuhusu taratibu za kukabidhiana watuhumiwa miongoni mwa mataifa ya Umoja wa Ulaya.

Maandamano yalikuwa yamepangwa katika mji wa kaskazini mwa Ujerumani wa Neumuenster, ambako Puigdemont alishikiliwa tangu kukamatwa kwake, kupinga uwezekano unaondelea kuzingatiwa wa kumkabidhi kwa Uhispania.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/dpa,afpe,ape

Mhariri: Yusra Buwayhid

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com