Profesa Wangari Maathai afariki dunia | Masuala ya Jamii | DW | 26.09.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Profesa Wangari Maathai afariki dunia

Maathai amefariki dunia jana jijini Nairobi baada ya kuugua saratani kwa muda mrefu. Kifo chake ni pigo kubwa kwa wanaharakati wa mazingira na bila shaka kwa ulimwengu kwa ujumla.

default

Profesa Wangari Maathai

Mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel, Wangari Maathai, ameaga dunia hospitalini alikokuwa akitibiwa saratani. Maathai alikuwa muasisi wa shirika la mazingira nchini Kenya, Kenya Green Belt Movemnet. Mkuu wa shirika hilo la mazingira, Karanja Njoroge, amesema Maathai alifariki dunia jijini Nairobi jana, jamaa na marafiki wakiwa kandoni mwake.

Wangari Maathai alikuwa kiongozi mashuhuri nchini Kenya tangu alipoanzisha shirika lake la mazingira mwaka 1977, akipigania kuhifadhi mazingira na utawala bora. Alishinda tuzo ya amani ya Nobel mwaka 2004 na kuwa mwanamke wa kwanza mwafrika, mkenya wa kwanza na mwanamazingira wa kwanza kutunukiwa tuzo hiyo. Shirika lake limepanda miti takriban milioni 40 kote barani Afrika. Bi Maathai pia aliwahi kuliongoza shirika la msalaba mwekundu nchini Kenya katika miaka ya 1970.

Wangari Maathai

Wangari Maathai akipanda miti

Bi Maathai alikuwa mwanaharakati wa haki za kiraia na haki za wanawake. Mbali na kazi yake ya kuyalinda mazingira aliwahi kuwa mbunge mnamo mwaka 2002 na baadaye kuteuliwa naibu waziri wa mazingira, wadhifa alioushikilia kati ya mwaka 2003 na 2005.

Kwa zaidi ya muongo mmoja kuanzia miaka ya 1980, shirika lake pia lilijiunga na vuguvugu la kupinga utawala wa mkono wa chuma wa rais wa zamani wa Kenya, Daniel arap Moi, huku mwanaharakati huyo akipigwa na polisi na kushambuliwa kwa mabomu ya kutoa machozi.

Kenia ehemaliger Präsident Daniel arap Moi

Rais wa zamani wa Kenya, Daniel arap Moi

Wakati huo alifanya kampeni ya kupinga ujenzi wa majengo mawili katika bustani ya Uhuru, kuzuia wizi wa misitu nje ya jiji la Nairobi na kufaulu kushinikiza wafungwa wa kisiasa 51 kuachiwa huru. Katika miaka ya hivi karibuni, alianzisha makundi ya kulinda mazingira na kuzindua kampeni kadhaa dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi na kuyalinda mazingira.

Nje ya Kenya, Wangari Maathai alijihusisha na juhudi za kuukoa msitu wa bonde la Kongo, msitu wa pili kwa ukubwa duniani ulio ni chanzo cha mvua. Maathai, aliyekuwa ametalakiana na mumewe, amewaacha watoto watatu na mjukuu mmoja wa kike.

Taarifa iliyotolewa na shirika lake imesema kuondoka kwa profesa Maathai hakukutarajiwa na ni pigo kubwa kwa kila mtu aliyemfahamu kama mama na mfanyakazi shupavu. Ni mfano bora wa kuigwa, shujaa na mtu aliyependa ukakamavu wake wa kuufanya ulimwengu kuwa na amani zaidi na mahala pazuri pa kuishi.

Mwandishi: Josephat Charo/afp/´reuters

Mhariri: Hamidou Oummilkheir

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com