Pompeo aitaka Iraq kusikiliza madai ya waandamanaji | Matukio ya Kisiasa | DW | 02.11.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Pompeo aitaka Iraq kusikiliza madai ya waandamanaji

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo amesema serikali ya Iraq inapaswa kuyasikiliza madai halali ya watu wanaoandamana kupinga rushwa na ukosefu wa ajira.

Pompeo amesema Marekani inafuatilia kwa karibu hali nchini Iraq. Katika taarifa yake, mwanadiplomasia huyo amesema pia uchunguzi wa Iraq kuhusu ghasia zilizozuka mwanzoni mwa mwezi Oktoba, haukuwa wa kuaminika na kwamba watu wa Iraq wanastahili kupata haki ya kweli.

Zaidi ya watu 250 wameuawa kutokana na maandamano hayo yaliyozuka Oktoba 1 yanayotaka pia kuimarishwa kwa huduma za serikali pamoja na kujiuzulu kwa Waziri Mkuu wa Iraq, Adel Abdel Mahdi. Watu wengine wanaokadiriwa kufikia 10,000 wamejeruhiwa na vikosi vya usalama.

Hayo yanajiri wakati ambapo siku ya Ijumaa maelfu ya watu walikusanyika katika Uwanja wa Tahrir, wengi wakiwa wanapeperusha bendera za Iraq wakiitaka serikali kujiuzulu na bunge kuvunjwa. Maandamano hayo yameingia mwezi wake wa pili sasa.

Watu wapatao 350 walijeruhiwa katika maandamano ya Ijumaa, baada ya vikosi vya serikali kufyatua risasi za mpira na mabomu ya kutoa machozi kwa lengo la kuwafukuza waandamanaji kwenye madaraja yanayoelekea katika eneo ambalo kuna ofisi za serikali ya Iraq na balozi za mataifa ya kigeni, maarufu kama Green Zone.

Wakati huo huo, kiongozi wa kidini wa madhehebu ya Shia nchini Iraq, Ayatollah Ali al-Sistani, ameonya kuhusu mataifa ya kigeni yenye nguvu kuingilia maandamano yanayoendelea ya kuipinga serikali.

Al-Sistani amesema Iraq haipaswi kutumbukizwa kwenye shimo la mauaji. ''Hakuna mtu au kundi, hakuna upande wala maoni fulani, hakuna mpatanishi wa kikanda au kimataifa anayepaswa kuyachukua madai ya watu wa Iraq na kuingiza matakwa yake,'' alisisitiza al-Sistani.

Matamshi hayo yametolewa siku moja baada ya kiongozi mkuu wa kidini wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei kuzitaka Iraq na Lebanon kulifanya suala la usalama kuwa kipaumbele chao. Amezitaka nchi hizo kudai matakwa yao kupitia mfumo wa kisheria.

Waandamanaji waikosoa Iran

Hata hivyo, waandamanaji mjini Baghdad walikosoa vikali uingiliaji wa Iran katika masuala ya ndani ya Iraq, baada ya al-Sistani kuzionya nchi za kigeni kutoingilia maandamano hayo. ''Hakuna mtu yeyote anayewawakilisha watu, sio Iran, sio vyama, sio viongozi wa kidini. Tunataka kuirudisha nchi yetu,'' alifafanua Ali Ghazi, mmoja wa waandamanaji hao.

Iraq imekuwa na uhusiano wa karibu lakini mgumu na Iran, jirani yake mkubwa wa mashariki pamoja na Marekani ambayo inapinga ushawishi wa Iran katika ukanda huo.

Iran iliibuka kama mpatanishi mkubwa nchini Iraq baada ya Saddam Hussein kuondolewa madarakani mwaka 2003. Iran inaiunga mkono serikali ya Iraq iliyoko madarakani na inaendeleza uhusiano wa karibu na makundi ya wanamgambo yanayoungwa mkono na serikali.

Siku ya Alhamisi, Rais wa Iraq, Barham Salih alisema Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Abdel-Mahdi yuko tayari kujiuzulu katika juhudi za kutekeleza madai ya waandamanaji wanaoipinga serikali.

Akilihutubia taifa kupitia televisheni, Salih alisema Mahdi alielezea nia yake ya kuwasilisha barua ya kujiuzulu na ameyataka makundi yote ya kisiasa kukubaliana kuhusu njia mbadala za kuzuia pengo la kikatiba. Rais huyo alisema ataidhinisha uchaguzi wa mapema baada ya kupitishwa rasimu mpya ya sheria ya uchaguzi.

Ama kwa upande mwingine, shirika la kimataifa la haki za binaadamu, Amnesty International limesema vikosi vya usalama mjini Baghdad vilifyatua mabomu ya kutoa machozi moja kwa moja kwenye umati wa watu na kusababisha majeraha ya kutisha.

Kwa mujibu wa shirika hilo wakati wa siku za mwanzo za maandamano hayo, karibu watu 150 waliuawa chini ya wiki moja baada ya vikosi hivyo kuwalenga waandamanaji kichwani na kifuani.

(AP, AFP, DPA)