Papa Leo akemea ukoloni wa kupora madini Afrika
21 Aprili 2026
Kiongozi wa kanisa katoliki duniani,Papa Leo wa XIV(14) amelaani ukoloni wa kuyapora madini ya bara la Afrika pamoja na migogoro inayoliandama bara hilo.Kiongozi huyo wa kiroho ameyasema hayo akiwa nchini Guinea ya Ikweta, kituo cha nne na cha mwisho cha ziara yake barani Afrika.
Akishangiliwa na umma wa waumini na wananchi wa taifa hilo lenye wakaazi wengi Wakatoliki Papa aliwasili katika mji mkuu Malabo akiwa amevalia kofia yake rasmi ya kipapa ya rangi nyekundu,hiyo ikiwa ni ziara ya kwanza kuwahi kufanywa na kiongozi mkuu wa kanisa katoliki nchini humo tangu mwaka 1982, alipotembelea St John wa Pili.
Katika ujumbe wake Guinea ya Ikweta nchi ambayo kiongozi wake amekaa madarakani tangu mwaka 1979 na akiwakandamiza wapinzani wake, Papa amelaani kile alichokiita ukoloni wa kuyadhibiti madini ya bara la Afrika na kiu ya kuwania madaraka.
Koloni hilo la zamani la Uhispania katika pwani ya Afrika Magharibi inaongozwa na rais Teodoro Obiang Nguema,kiongozi aliyekaa muda mrefu madarakani barani Afrika anayelaumiwa kueneza ufisadi na kuendesha utawala wa kimabavu.
Pamoja na utajiri wa mafuta uliogunduliwa katika taifa hilo katikati ya miaka ya 1990 uliobadilisha hali ya uchumi, zaidi ya nusu ya wananchi wa taifa hilo lenye wakaazi karibu milioni 2 wanaoshi kwenye umasikini.
Papa Leo aliyewasili nchini humo akitokea Angola amekutana na rais Obiang katika ikulu na kisha kutowa hotuba mbele ya maafisa wa serikali, wanadiplomasua na wawakilishi wa mashirika ya kiraia.
Na katika hotuba hiyo ambayo imekwenda sambamba na siku ya kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu kifo cha Papa Francis, kiongozi huyo wa kiroho alitumia maneno yaliyowahi kusemwa na mtangulizi wake huyo ya kulaani ukosefu wa usawa kwenye mapato.
Papa Leo XIV amesema kukosekana usawa kwenye kutoa mapato, kumezidishwa na hali ya uchumi wa dunia unaojikita zaidi katika kutafuta faida bila kujali wengine.
Papa leo pia amegusia namna ambavyo matatizo yameongezeka na kushuhudiwa waziwazi hivi sasa kuliko miaka iliyopita , kwa kuitaja migogoro ya kivita inayoshuhudiwa mara kwa mara ikichagizwa na ukoloni wa kutaka kupora mafuta na madini bila ya kujali sheria ya kimataifa au sauti za wananchi wanaopinga.
Guinea ya Ikweta ni nchi ambayo haiongozwi kwa misingo ya dini lakini kiasi asilimia 75 ya wakaazi wake ni Wakatoliki na hivyo kuifanya kuwa nchi yenye idadi kubwa zaidi ya waumini wakotoliki barani Afrika.
Kesho Jumatano Papa Leo atatembelea gereza lililoko katika mji wa bandari wa Bata na kukamilisha ziara yake Alhamisi kwa kufanya misa kubwa katika uwanja wa michezo wa Malabo.