1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan Kusini

Papa Francis yu njiani kuelekea nchini Sudan Kusini

Jean Noël Ba-Mweze
3 Februari 2023

Papa Francis anaelekea Sudan Kusini baada ya kukamilisha ziara yake ya siku nne nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

https://p.dw.com/p/4N3Pc
DR Kongo Papstmesse in Kinshasa
Picha: Jerome Delay/AP Photo/picture alliance

Akiwa Congo alikutana na watu wa matabaka mbalimbali na kuwahubiri kuhusu amani, umoja, msamaha na kupambana dhidi ya ufisadi. Lakini baada ya mkutano wake na vijana jana Alhamisi, mabishano sasa yanaendelea baina ya mamlaka na upinzani.

Wakati Papa Francis alipowahutubia vijana hao hasa alipowaomba kukataa aina zozote za ufisadi, vijana  waliimba nyimbo dhidi ya Rais Félix Tshisekedi wakimkumbusha kuwa muda wake wa uongozi tayari umekwisha, jambo ambalo linalaumiwa na vyama vilivyo madarakani na kuushutumu upinzani kwa kuwatumia vijana hao.

Malumbano ya kisiasa baina ya serikali na upinzani Congo kufuatia mikutano ya Papa

"Hatupaswi kugeuza shughuli ya kidini kuwa ya kisiasa. Sote tumeona hapo bendera za vyama vya kisiasa, bendera za wapinzani. Waliwatumia vijana hawo ila ni muhimu kujua kwamba muhula wa rais bado unaendelea. Jambo muhimu kwetu ni ziara ya Papa ambayo imefanikiwa kwani Kongo imeweza kusikika," amesema Trésor Mwamba ambaye ni mmoja wa viongozi wa UDPS, chama cha Rais Félix Tshisekedi.

Shutuma hizo hata hivyo zimetupiliwa mbali na upinzani wakisema vijana hao walimueleza tu Papa ukweli wa hali ambayo Wakongo wanapitia kufuatia uongozi wa Félix Tshisekedi hapa Kongo.

Papa awaasa vijana Kongo

Robert Maungano Kihyoka, mmoja wa viongozi wa muungano wa upinzani wa Lamuka amesema "Hawa watu wa Félix yawezekana wanaishi nje ya Kongo. Namna gani nchi itatawaliwa na Rwanda na Mkongo abakie kimya? Namna gani wakongo watakufa na njaa Mukongomani abaki kimya ? Hiyo ni kusema kwamba Wakongo wameishachoka na wasingekuwa wavumilivu, Félix hangelipaswa tena kutawala Kongo."

Papa Francis kukutana na vijana wa Kongo

Katika kipindi chote cha ziara yake mjini Kinshasa, Papa Francis alisisitiza amani, umoja, msamaha na alikemea vita dhidi ya ufisadi nchini Kongo.

Mkuu huyo wa Kanisa Katoliki ulimwenguni tayari amemaliza ziara yake Congo Ijumaa na kuondoka Kinshasa kuelekea Juba nchini Sudan Kusini.