1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Francis awasili Kongo, akianza ziara ya siku sita

Sylvia Mwehozi
1 Februari 2023

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis amewasili nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuanza ziara itakayoangazia athari za mzozo wa muda mrefu kwenye taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa madini.

https://p.dw.com/p/4MuyI
DRK Kongo Papst Franziskus
Picha: REUTERS

Papa Francis ni kiongozi wa kwanza wa kanisa hilo la Katoliki kutembelea Jamhuri wa Kidemokrasia ya Kongo, tangu mara ya mwisho alipozuru Papa John Paul II mwaka 1985, wakati huo ikiitwa Zaire. Karibu nusu ya idadi ya watu wa nchi hiyo yenye watu karibu milioni 90 ni Wakatoliki.

Baada ya hafla ya kumkaribisha na kukutana na rais Felix Tshisekedi, kiongozi huyo wa Kanisa, mwenye miaka 86 atatoa hotuba kwa viongozi, wanadiplomasia na wawakilishi wa taasisi zisizo za kiraia.

"Kwangu mini, ni mara ya kwanza kumuona Papa kwa macho yangu.. mara nyingine namuona tu kwenye runinga. Ni furaha kubwa sana kwangu," amesema Alain Difima padri wa Katoliki aliyekaa muda mrefu katika uwanja wa ndege akisubiri ndege ya kiongozi huyo kutua.

Ujumbe wa Papa Francis umewasili jijini Kinshasa Pamoja na ujumbe mkuu wa Papa Francis huyo kwenye ziara hiyo kuwa ni amani lakini pia analenga kukabiliana na dhana ya kikoloni kwamba bara la Afrika liko tayari kunyonywa.

Kituo cha kwanza cha kiongozi huyo kitakuwa mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo-Kinshasa atakakokaa hadi siku ya Ijumaa. Kisha Francis ataelekea mjini Juba kabla ya kurejea Vatican siku ya Jumapili.

DRK Kongo Papst Franziskus
Raia wengi nchini humo wamejitokeza kumlaki Papa francis mara baada ya kuwasili mjini Kinshasa mchana wa leo.Picha: REUTERS

Mashirika ya misaada yanatumai ziara ya Francis itamulika mizozo iliyosahauliwa ya mataifa na kuamsha tena nadhari ya kimataifa kuhusu mizozo mibaya zaidi ya kibinadamu barani Afrika katikati mwa uchovu wa wahisani na vipaumbele vipya vya misaada nchini Ukraine.

Soma Zaidi: Papa Francis akutana na kiongozi wa jeshi la Myanmar

Mikoa ya mashariki mwa Kongo katika siku za hivi karibuni imeshuhudia ongezeko la machafuko baina ya waasi na vikosi vya usalama vya serikali. Katika nchi jirani ya Sudan Kusini ambayo ilipata uhuru wake mwaka 2011 kutoka Sudan, kumekuwa na makabiliano ya mara kwa mara baina ya makabila hasimu. Nchi zote mbili pia zimeathirika na mabadiliko ya tabia nchi zikiathiriwa na mafuriko ya hivi karibuni.

Ziara ya Papa pia itamleta uso kwa macho na mustakabali wa Kanisa Katoliki, katika bara ambalo ni moja ya maeneo pekee ambako kundi la waumini wa Kanisa Katoliki linakua, katika muktadha wa ufanyaji ibada pamoja na miito mipya ya ukasisi na maisha ya kidini.

Kiongozi huyo pia anatarajiwa kufanya ibada ya umma katika kambi ya jeshi la anga mjini Kinshasa siku ya Jumatano ambayo huenda ikawakusanya waumini milioni moja pamoja na kukutana na wahanga wa machafuko na wakimbizi.

Soma Zaidi: Papa awatangaza John wa 23 na John wa Pili watakatifu