1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Francis akwepa kuwataja "Warohingya" Myanmar

Mohammed Khelef
28 Novemba 2017

Mkuu wa Kanisa Katoliki, Papa Francis, ametaka haki na heshima kwa haki za binaadamu kwenye hotuba yake muhimu kabisa nchini Myanmar, ingawa amekwepa kutaja chochote kuhusu Warohingya wanaokandamizwa.

https://p.dw.com/p/2oOeo
Myanmar Papst Franziskus bei Aung San Suu Kyi in Naypyitaw
Picha: Reuters/M. Rossi

Akiwa jukwaa moja na kiongozi mkuu wa Myanmar, Aung San Suu Kyi katika mji mkuu, Naypyidaw, Papa Francis hakulitaja kabisa suala la mgogoro wa Warohingya, na badala yake akaamuwa kulifungafunga kwenye haja jumla ya haki, heshima na utawala wa sheria kwa kila mmoja nchini humo.

"Mustakabali wa Myanmar unapaswa kuwa amani, amani iliyojikita kwenye misingi ya heshima kwa utu na haki za kila mwanajamii, heshima kwa kila kundi la kijamii na utambulisho wake, heshima kwa utawala wa sheria, na heshima kwa utaratibu wa kidemokrasia unaomuzesha kila mtu na kila kundi - bila kutengwa - kutoa mchango wake halali kwa maslahi ya wote," alisema Papa Francis.

Hata hivyo, shirika la habari la AP linasema maneno haya yalikuwa ni uungwaji mkono wa kimya kimya wa Warohingya, ambao wamekuwa wahanga wa miongo mingi ya ukandamizwaji wa dola na mashambulizi ya hivi karibuni ambayo Umoja wa Mataifa unayaelezea kama mfano wa kitabuni wa kampeni ya safishasafisha dhidi ya jamii.

Aepuka neno "Rohingya"

Papa Francis akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa kidini mjini Yangon, Myanmar.
Papa Francis akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa kidini mjini Yangon, Myanmar.Picha: Reuters/Osservatore Romano

Lakini neno halisi "Rohingya", ambalo linachukuliwa na waumini wa Buddha walio wengi nchini humo, kuwa matusi dhidi yao, halikuwamo kabisa kwenye hotuba nzima ya Papa Francis.

Utawala wa Mnyanmar ukiungwa mkono na waumini wa Buddha wanawaita Waislamu hawa wasiotambuliwa na taifa lolote kuwa raia kamili, kuwa ni wahamiaji wa "Kibengali", wakimaanisha raia wa Bangladesh, taifa jirani lenye kukaliwa na Waislamu wengi, na ambalo tangu mwezi Agosti hadi sasa limeshawapokea Warohingya zaidi ya 600,000.

Mashirika ya haki za binaadamu yalikuwa yanamshinikiza Papa Francis kukemea vikali mateso dhidi ya Warohingya kwenye ziara yake ya siku nne, lakini viongozi wa Kanisa lake nchini humo walikwishamtahadharisha na mapema dhidi ya kujiingiza kwenye suala hilo. 

Kwa upande wake, Suu Kyi, mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel, alizungumzia changamoto zinazoikabili nchi yake baada ya miongo mitano ya utawala wa kijeshi, lakini naye pia hakugusia kabisa suala la Rohingya.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AP/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman