1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Benedict XVI ziarani Poland

Josephat Charo25 Mei 2006

Kiongozi wa kanisa katoliki papa Benedict XVI ameanza ziara yake ya siku nne nchini Poland hii leo. Anaitembelea nchi ya kiongozi wa zamani wa kanisa hilo, Yohana Paulo II katika ziara itakayomleta karibu na wapoland walioteswa na manazi wa Ujerumani wakati wa vita vya pili vya dunia.

https://p.dw.com/p/CHLT
Baba mtakatifu Benedict XVI (kushoto) na rais wa Poland Lech Kaczynski
Baba mtakatifu Benedict XVI (kushoto) na rais wa Poland Lech KaczynskiPicha: AP

´Nimekuja kufuata nyayo za Yohana Paulo II, kuifuata njia ya maisha yake,´ amesema papa Benedict XVI kwa lugha ya kipoland alipowasili katika uwanja wa ndege wa Okecie, mjini Warsaw.

Papa Benedict XVI anasema ana furaha kuitembela Poland. Imekuwa azma yake kulitebelea taifa anakotoka kiongozi aliyemrithi, Yohana Paulo II na kuwa pamoja na wapoland. Ameongeza kusema kwake hiyo sio ziara tu ya kawaida ila ni safari ya imani katika maisha ya kiroho.

Papa alishangiliwa kwa nderemo na vifijo na wafanyikazi wa uwanja wa ndege wa Okecie na viongozi mashuhuri waliokuja kumlaki. Upepo mkali ulilipeperusha joho lake leupe alipokuwa akishuka kutoka ndege ya shirika la ndege la Alitalia. Kwaya ya wafanyikazi wa uwanja wa ndege wa Okecie mjini Warsaw iliimba nyimba za kumsifu Mungu.

Rais wa Poland Lech Kaczynski, kadinali Jozef Glemp na askofu mkuu wa Krakow Stanislaw Dziwisz, walikuwa miongoni mwa viongozi waliomlaki kiongozi huyo.

Rais Kaczynski amemwambia papa Benedict XVI kwamba ilikuwa mpango wa Mungu kwa mjerumani kuchukua hatamu za uongozi wa kanisa katoliki baada ya raia wa Poland Yohana Paulo II kuaga dunia. Wajerumani na wapoland ambao ni majirani mara kwa mara wakekuwa wakitengwa na historia mbaya ya vita. Raia Kaczynski amesema,

´Tunamsalimu baba mtakatifu kwa heshima kuu, kwa furaha na kwa matumaini makubwa. Kama rais wa Poland na mkatoliki, ninafuraha sana na ninajivunia kwamba umeichagua Poland kama kituo chako cha kwanza katika ziara zako. Tunakushukuru sana baba mtakatifu kwa kuja kutujenga kiimani.´

Kutoka uwanja wa ndege papa Benedict XVI alilitembelea kanisa la St Johns lililo katikati ya mji wa Warsaw. Njiani alitoa heshima zake kwa mashujaa wa Poland wa mwaka wa 1943 waliouwawa walipojaribu kupigana na manazi wa Ujerumani walioikalia Poland wakati wa vita vya pili vya dunia. Alionyesha ishara ya kubariki gari lake lilipokuw likipita mnara wa ukumbusho.

Lakini jambo liliwavunja moyo watu wengi waliokuwa wamesimama mahala hapo ni kwamba gari la papa halikupunguza mwendo wala kusimama kumuwezesha kushuka na kutoa heshima zake kwa wayahudi walioteswa mjini Warsaw wakati wa vita. Ni jambo la kuhuzunisha kwamba amepita haraka, amesema Zofia Sienienska, raia wa Poland aliyetunzwa kw akuyahatarisha maisha yake akijaribu kuwaokoa wayahudi wakati wa mauaji ya Holocaust.

Hatah hivyo kuhani mkuu wa kiyahudi nchini Poland, Michael Schudrich ameliambia shirika la hagari la AFP kwamba kwa papa Benedict XVI kulitembelea eneo hilo na kutoa ishara ya kubariki katika utamaduni wa dini ya kikatoliki, ni jambo muhimu.

Maelfu ya wapoland walikusanyika katika barabara za mji wa Warsaw kumkaribisha Benedict XVI. Wengi walipiga kele za kumtakia maisha marefu huku wengine wakibeba bendera ya makao makuu ya kanisa katoliki, Vatican. Kiongozi huyo pia alipitia mbele ya mnara mwingine wa kuwakumbuka wapoland waliofukuzwa na kuuwawa katika muungano wa zamani wa Sovieti na mnara mwingine kwa wapoland waliopinga manazi wa Ujerumni mwaka wa 1944.

Mji wa Warsaw uliharibiwa kabisa wakati vita vilipokaribia kumalizika, na wayahudi takriba milioni 3.5 waliokuwa wakiishi nchini humo waliangamizwa. Kama vijana wengi wa Ujerumani, Benedict alisajiliwa katika kundi la vijana wa Hitler, lakini hakushiriki katika mapigano na baadaye akalihama jeshi la Hitler