1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ntaganda atiwa hatiani na mahakama ya ICC

Josephat Charo
8 Julai 2019

Mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ya ICC mjini The Hague imemtia hatiani mbabe wa zamani wa kivita wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Bosco Ntaganda kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu na uhalifu wa kivita.

https://p.dw.com/p/3Lk5N
Niederlande Internationaler Gerichtshof Prozess Bosco Ntaganda Den Haag
Picha: Getty Images/AFP/ANP/B. Czerwinski

 

Ntaganda, ambaye alishikilia hana hatia wakati wa kipindi cha miaka mitatu ya kusikilizwa kwa kesi dhidi yake, anakabiliwa na kifungo cha maisha jela baada ya kukutikana na hatia leo katika mahakama ya kimataifa ya ICC. Hakuonyesha hisia zozote wakati jaji aliyesimamia kesi hiyo, Robet Fremr, alipopitisha hukumu hiyo. Ntaganda alitiwa hatiani mara ya kwanza mnamo mwaka 2006 na kuwa ishara ya kufanya uhalifu bila hofu ya kuchukuliwa hatua kisheria katika bara la Afrika, akihudumu kama jenerali katika jeshi la Congo kabla kujisalimisha mwaka 2013 wakati nguvu zake ziliposambaratika.

Ntaganda mwenye umri wa miaka 45 alishtakiwa kwa kusimamia mauaji ya raia na wanajeshi wake katika eneo linalokabiliwa na machafuko na lenye utajiri wa madini la Ituri mashariki mwa Jamhuri ya Kidemkorasia ya Congo mnamo mwaka 2002 na 2003.

Waendesha mashitaka walitoa taarifa za kina za kutisha za wahanga wakiwamo baadhi waliopasuliwa matumbo na koo zao, kama sehemu ya ushahidi katika kipindi cha miaka mitatu ya kusikilizwa kwa kesi yake katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ya ICC mjini The Hague.

Ntaganda, aliwaambia majaji wakati wa kesi yake kwamba alikuwa mwanajeshi na wala sio muhalifu na kwamba jina la utani la "Terminator" halimhusu. Mzaliwa huyo wa Rwanda anakabiliwa na mashitaka 13 ya uhalifu wa kivita na mashitaka matano ya uhalifu dhidi ya ubinadamu kwa jukumu lake wakati wa machafuko ya kinyama yaliyotokea eneo la kaskazini mashariki mwa Congo. Mashitaka hayo yanajumuisha mauaji, ubakaji, kuwasajili watoto kama wanajeshi na kuwanyanyasa kingono, uporaji na kuwalazimisha raia kuyakimbia makazi yao. Ntaganda ameyakanusha mashitaka yote dhidi yake katika kesi inayomkabili, ambayo ilianza kusikilizwa mnamo Septemba 2015 mjini The Hague.

Ntaganda alikuwa kiongozi katili

Waendesha mashitaka wanasema uhalifu huo ulifanyika wakati Ntaganda alipoliongoza kundi la Patriotic Forces for the Liberation of Congo, FPLC, bawa la kijeshi la chama cha Union of Congolese Patriots, katika jimbo la Ituri, kaskazini mashariki mwa Congo kati ya mwaka 2002 na 2003.

Waendesha mashitaka pia walimueleza Ntaganda kama kiongozi asiye huruma wa uasi wa Watutsi wakati wa vita vilivyoiyumbisha Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo baada ya mauaji ya halaiki ya 1994 katika taifa jirani la Rwanda.

Watu zaidi ya 60,000 wameuliwa tangu machafuko yalipozuka katika eneo hilo mnamo mwaka 1999 kwa mujibu wa mashirika ya kutetea haki za binadamu, wakati waasi wapipokabiliana kupigania udhibiti wa raslimali ya madini.

Ntaganda pia alishirikishwa na vuguvugu la M23, ambalo lilisaini mkataba wa amani na serikali ya Congo mwaka 2013. Alijisalimisha mwenyewe kwa ubalozi wa Marekani katika mji mkuu wa Rwanda, Kigali, mwaka 2013 baada ya kuepuka mitego ya kumkamata kwa miaka saba.

Kamanda wa zamani Ntaganda, Thomas Lubanga, alihukumiwa kifungo cha miaka 14 mwaka 2012 kwa kuwatumia wanajeshi watoto, na hivyo kuwa mtu wa kwanza kutiwa hatiani na mahakama ya ICC.