Majaji kusikiliza hoja za mwisho kesi dhidi ya Ntaganda | Matukio ya Afrika | DW | 28.08.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Majaji kusikiliza hoja za mwisho kesi dhidi ya Ntaganda

Majaji katika mahakama ya kimataifa ya jinai na uhalifu wa kivita ICC , wanaanza kusikiliza hoja za mwisho katika kesi dhidi ya mbabe wa zamani wa vita katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Bosco Ntaganda.

 Akijulikana wakati mmoja kwa jina la utani la "Terminator",yaani mmalizaji Ntaganda anakabiliwa na makosa 13 ya uhalifu wa kivita na matano ya uhalifu dhidi ya binadamu,  kwa ajili ya jukumu lake kwenye  mgogoro wa kikatili wa vita ya wenyewe kwa wenyewe katika eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo zaidi ya miaka 15 iliyopita. Ntaganda ambaye ana asili ya Rwanda mnamo mwezi Septemba 2015 alikanusha kuhusika na uhalifu huo mwanzoni mwa kesi yake mbele ya mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC.

Waendesha mashitaka katika mahakama ya ICC iliyoko mjini the Hague, wanasema jeshi lake la waasi kati ya mwaka 2002 na 2003 lilifanya utawala wa hofu katika mkoa wa kaskazini mashariki wa Ituri, na kusababisha unyanyasaji wa kutisha dhidi ya wenyeji.

Ntaganda alipanga operesheni za jeshi lake la Patriotic Forces for the Liberation of Congo (FPLC), akiwatumia watoto kama askari na kuwalazimisha wanawake katika utumwa wa ngono wakati akiwashambulia raia kwa misingi ya kikabila. Fatou Bensouda ni mwendesha mashitaka mkuu wa ICC, na anasema " Bosco Ntaganda, kamanda maarufu anayejulikana kama Terminator yuko hapa mbele yako kwa ajili ya jukumu lake kutekeleza kampeni ya vurugu na hofu, dhidi ya raia na watoto."

Bosco Ntaganda Prozess ICC Den Haag 10.01.2014 Bensouda (Reuters)

Mwendesha mashitaka mkuu wa ICC Fatou Bensouda

Kamanda huyo mwenye haiba kubwa, na Jenerali wa zamani mwenye kuogopwa alitoa maagizo, kupanga itifaki na silaha kwa vikosi vyake wamesema waendesha mashitaka. Watu kiasi ya  800 waliuawa na jeshi la FPLC wakati lilipopambana na wanamgambo hasimu kwa ajili ya udhibiti wa maeneo yenye utajiri wa madini.

Waendesha mashitaka wamemtaja Ntaganda pekee kwa madai ya kuongoza shambulio la mwaka 2002 kwenye mji wenye mgodi wa dhahabu wa Mongbwalu, shambulio lililodumu kwa siku sita na kuwaua wanakijiji 200.

Ntaganda aliye na umri wa miaka 44, wakati wa kesi yake alisita kulikubali jina lake la utani la Terminator na kuwaeleza majaji kwamba yeye alikuwa ni "askari, na sio mhalifu", akiongeza kwamba hakuwahi kuwashambulia raia badala yake aliwalinda.

"Nakanusha kuhusika na uhalifu ambao mmejulishwa hapa", alisema Ntaganda.

Ntaganda ni mtuhumiwa wa kwanza kujisalimisha katika mahakama ya ICC, mwaka 2013 alikwenda mwenyewe katika ubalozi wa Marekani mjini Kigali na kuomba apelekwe mahakamani.

DRC Rebellenführer Jean Bosco Ntaganda (dapd)

Bosco Ntaganda akiwa katika sare zake za kijeshi akiwa

Kamanda huyo wa zamani ndiye mwanzilishi wa kundi la waasi la M23, ambalo lilitokomezwa na vikosi vya jeshi la Congo miaka mitano iliyopita.

Mapigano katika eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, yamewaua watu karibu 60,000 tangu mwaka 1999, yakichangiwa na utajiri wa rasilimali ya madini katika mkoa huo, hususan dhahabu na madini yanayotumika katika bidhaa za kielektroniki.

Kesi ya leo itaendelea hadi siku ya Alhamis, ambapo Ntaganda anatarajiwa kutoa kauli kuelekea mwishoni mwa kesi hiyo. Inaweza kuchukua miezi kadhaa , au hata miaka kabla ya majaji wa ICC hawajatoa hukumu. Kesi ya Ntaganda inatarajiwa kufuatiliwa kwa ukaribu baada ya kiongozi mwingine wa zamani wa Congo Jean-Pierre Bemba kuondolewa hatia na mahakama hiyo.

Awali alikuwa amehukumiwa miaka 18 jela kwa makosa ya uhalifu wa kivita yaliyotekelezwa na vikosi vyake huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, Bemba aliachiwa huru baada ya kushinda rufaa mwezi Juni na kisha kurejea Kinshasa.

Hata hivyo Kamanda wa zamani wa jeshi la FPLC Thomas Lubanga alihukumiwa miaka 14 jela mwaka 2012, ikiwa ni hukumu ya pili kutolewa na mahakama hiyo tangu ilipoanzishwa miaka 16 iliyopita.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman