Niger yachagua vita dhidi ya Boko Haram | Matukio ya Afrika | DW | 10.02.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Niger yachagua vita dhidi ya Boko Haram

Bunge la Niger limepiga kura kwa kauli moja, kutuma vikosi nchini Nigeria kujiunga na mapambano ya kikanda dhidi ya kundi la Boko Haram. Kulingana na azimio la bunge hilo, Niger itatuma wanajeshi 750 nchini Nigeria.

Wavuvi hawaendi tena ziwani kuvua, wakulima hawaendi tena mashambani, shule zimefungwa. Wakaazi wa maeneo ya mpakani ya Diffa na Bosso, kusini mwa Niger wamejawa na hofu, kutokana na magaidi waliojigeuza wapiganaji wa jihadi, ambao wanatishia usalama wa taifa lao." Hao ni makatili tu wasioheshimu sheria, wanaiba, kuuwa, na kubaka," alisema Abdou Lokoko, mfanyakazi wa shirika lisilo la kiserikali nchini Niger.

Kwa mara ya kwanza wapiganaji hao kutoka kaskazini mwa Nigeria wameshambulia maeneo ya upande wa Niger katika siku chache zilizopita. Siku ya Jumatatu, wakati bunge likijiandaa na kura hiyo, Boko Haram waliushambulia mji wa Diffa wenye wakaazi 60,000 na kuuwa watu watano.

Wanajeshi wa Chad wanaopambana na Boko Haram nchini Nigeria.

Wanajeshi wa Chad wanaopambana na Boko Haram nchini Nigeria.

Jeshi lilifanikiwa kuwafurusha, kwa mujibu wa maelezo yake, lakini muda mfupi baadae, ilifuatia miripuko ya mabomu.Katika mashambulizi sawa na hayo wiki iliyopita, mamia ya wapiganaji wa Boko Haram waliripotiwa kuuawa katika miji ya Diffa na Bosso, pia wanajeshi kadhaa na raia pia walipoteza maisha.

"Tuna ushahidi wa Boko Haram kuendesha harakati zake ndani ya Niger, na hiyo ni tangu mwaka 2012, wakati washukiwa kadhaa wa Boko harama walipokamatwa na maafisa wa idara ya usalama ya Niger, hasa katika mikoa wa Zinder na Diffa iliyoko mpakani na Nigeria," alisema Ryan Cummings, mchambuzi wa masuala ya usalama wa shirika la ushauri la red.24 la Afrika Kusini, ambalo ni sehemu ya mtandao wa usalama wa Nigeria.

Kikosi cha pamoja dhidi ya Boko Haram

Mwishoni mwa wiki Nigeria na majirani zake - Chad, Niger, Cameroon na Benin, zilikubaliana kuunda kikosi cha wanajeshi, polisi na watalaamu wa kiraia 8,700, kwa ajili ya mapambano dhidi ya Boko Haram. Idadi hii ni kubwa kuliko iliyopendekezwa na Umoja wa Afrika. Tayari wanajeshi wa Chad wako katika eneo la mpakani wakipambana na Boko Haram tangu mwezi Januari. Cameroon nayo imeanza kujitayarisha.

"Yeyote anaetaka amani laazima ajiandae na vita hivi," alisema Abdou Lokoko, ambaye pamoja na shirika lake wamekuwa wakitoa wito wa kujenga kikosi cha pamoja dhidi ya Boko Haram. "Ikiwa hatutofanya chochote, basi wataendelea kutushambulia. Wanajeshi wetu ni mashujaa na wako tayari kwa mapambano. Mungu akipenda watatulinda."

Ramani inayoonyesha maeneo ambako wanajeshi wa Chad wanashaishambulia Boko Haram.

Ramani inayoonyesha maeneo ambako wanajeshi wa Chad wanashaishambulia Boko Haram.

Jeshi kamili la magaidi

Lakini kumuamini Mungu tu hakutowasaidia wanajeshi hao. Taarifa mpya za mashirika ya ujasusi ya Marekani zinaonyesha kuwa Boko Haram ina wapiganaji kati ya 4000 na 6000. Katika maeneo yaliyoko chini ya udhibiti wake, kundi hilo lina mtandao wa miji na vijiji 30, ambako linaweza kuwandikisha wapiganaji.

Idadi hii haimshangazi mtaalamu wa masuala ya usalama Ryan Cummings. Anasema huenda wapiganaji wa Boko Haram ni wengi zaidi kuliko idadi hiyo. "Hao ndiyo wale wapiganaji wa itikadi kali waliofunzwa vizuri. Kuna wapiganaji wa ziada, ambao ama wanaandikishwa kwa nguvu, au wanalipwa.Kuna uvumi pia kuwa kundi hilo linakodi magenge yenye silaha."

Kwa hilo kundi hilo la kigaidi limeunda jeshi kamili tangu muda mrefu. Na pia lina kiongozi anaependa kujionyesha kwa jamii kama mtu asiye na mzaha.Katika mkanda wake wa video wa karibuni, Abubakar Shekau anaonekana akiapa kukishinda vibaya kikosi hicho cha kanda.

"Tutamkamata mmoja baada ya mweingine," alitishia Shekau, akiyalenga mataifa yanayoshiriki operesheni dhidi ya kundi lake. Lakini Mchambuzi Ryan Cummings anaamini jeshi la pamoja litaweza kuidhofisha Boko Haram.

Kiongozi wa Boko Haram, Abubakar Shekau.

Kiongozi wa Boko Haram, Abubakar Shekau.

"Kundi hilo litalaazimika kwa mara ya kwanza kupambana kwenye nyanja tofauti kwa wakati mmoja. Hadi sasa Boko Haram ilikuwa inapambana na jeshi la Nigeria kutokea upande wa magharibi. Kwa nchi za Chad, Cameroon, Benin na Niger kujiunga na mapambano hayo, kundi hilo sasa litakabiliwa kwenye maeneo ya mashariki na kaskazini.

Changamoto zinazowakabili washirika

Lakini hilo linahitaji rasilimali: Wanajeshi, silaha, na vifaa vingine. Hilo litalipa kundi hilo changamoto kubwa na linaweza kudhoofisha kwa kiasi kikubwa, anasema Cummings. Lakini kikosi hicho cha kimataifa kinakabiliwa na changamoto kubwa sana. Ukosefu wa kuaminiana kati ya mataifa washirika, mizozo inayotokana na eneo lenye utajiri wa rasilimali kwenye ziwa Chad, ni vikwazo tosha.

Lakini suala la ufadhili haliko bayana. Umoja wa Mataifa ulitaka kushiriki kwa kuwezesha usafiri, Umoja wa Afrika ulikuwa bado haufikia uamuzi wowote.

Mwandishi: Julia Hahn
Tafsri: Iddi Ssessanga
Mhariri: Daniel Gakuba

DW inapendekeza

Matangazo

IJUE DW

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com