NEW YORK : Ban ahimiza usuluhishi Somalia | Habari za Ulimwengu | DW | 05.01.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Habari za Ulimwengu

NEW YORK : Ban ahimiza usuluhishi Somalia

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameihimiza serikali ya mpito ya Somalia hapo jana kutafuta suluhisho la kisiasa na kutowa wito wa kuwekwa kwa haraka kwa wanajeshi wa kulinda amani wa Afrika nchini humo.

Katibu Mkuu huyo mpya wa Umoja wa Mataifa anaamini kwamba kutimuliwa kwa wanamgambo wa Kiislam nchini humo katika kipindi cha siku 10 zilizopita kulikofanywa na vikosi vya serikali ya Somalia vikisaidiwa na vile vya Ethiopia kunatowa fursa mpya kwa serikali ya mpito kuweka mamlaka yake kikamilifu katika nchi nzima kwa mara ya kwanza kabisa.

Msemaji wa kike wa Umoja wa Mataifa Michele Montas amesema Ban amekaribisha taarifa ya Ethiopia kwamba inakusudia kuondowa vikosi vyake kwa haraka na amezitaka nchi zote katika eneo hilo kuheshimu mamlaka ya nchi hiyo, umoja wake na haki ya kujiamulia mambo yake yenyewe.

Wakati huo huo Rais Yoweri Museveni wa Uganda amesema Uganda iko tayari kutuma wanajeshi wa kulinda amani nchini Somalia mara tu baada ya bunge la nchi yake kuidhinisha mpango huo.

Rais Museveni alitowa kauli hiyo wakati wa mkutano wa pamoja wa waandishi wa habari na Waziri Mkuu wa Ethiopia Meles Zenawi mjini Addis Ababa hapo jana.

Maafisa wa serikali ya Uganda wamekuwa wakielezea wasi wasi wao mara kadhaa juu ya kutumwa kwa kikosi hicho kwenye nchi hiyo ya Pembe ya Afrika kwa kusema kwamba kikosi hicho kinahitaji kufafanuliwa majukumu yake nchini Somalia pamoja na kuwa na mkakati wa kujitowa nchini humo.

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com