Mwandishi wa habari China afungwa jela kuhusiana na Covid-19
21 Septemba 2025
Mwandishi wa habari wa China ambaye alifungwa jela kwa kuripoti mlipuko wa awali wa COVID-19, amehukumiwa tena adhabu ya kifungo cha miaka minne jela. Katika kesi mpya, mwandishi huyo Zhang Zhan alikamatwa Agosti mwaka 2024 kwa makosa ya kusababisha matatizo, mashtaka yanayotumiwa mara kwa mara na mamlaka kukandamiza upinzani. Shirika la waandishi wa habari wasio na mipaka RSF, limesema Zhang aliye na umri wa miaka 42 alitiwa mbaroni kufuatia kuripoti kwake juu ya ukiukwaji wa haki za binadamu na serikali ya China. Katika kesi iliyopita, Zhang alishikiliwa Mei mwaka 2020 baada ya kusafiri katika jiji la Wuhan, ambako alirekodi vidio kwa kutumia simu ya mkononi juu ya taharuki ya ugonjwa huo kwenye kitovu cha mlipuko na kuwahoji maafisi namna wanavyoshughulikia hali hiyo.