1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwanafunzi ashikiliwa kwa kumuuwa mwalimu Kenya

Daniel Gakuba
25 Januari 2019

Mwanafunzi mmoja anatuhumiwa kumuua mwalimu wake katika shule sekondari nchini Kenya. Mwanafunzi huyo wa kidato cha nne ni mmoja wa washukiwa watatu wanaotuhumiwa kwa tukio hilo.

https://p.dw.com/p/3CBbY
Kenia Schüler in Nakuru trauern um den Tod ihres Lehrers
Wanafunzi wakilia kuomboleza kifo cha mwalimu waoPicha: DW/W. Mbogho

Taarifa kutoka shuleni hapo zimeeleza kuwa marehemu Peter Omari aliyekuwa mwalimu wa somo la Fizikia jana Alhamis alimpokonya mwanafunzi wa kidato cha nne simu ya mkononi aliyokuwa amepewa na watu wawili kupitia ua la shule. Maafisa wa polisi wanaamini kuwa, watu hao wawili walipanga njama na mwanafunzi huyo kumuuwa mwalimu Omar kwa nia ya kulipiza kisasi, kwani inasemekana mwaka 2017 watu hao hao walikamatwa wakimpa mwanafunzi mwingine simu ya mkononi.

Chifu anayesimamia eneo la Barut David Kering anaeleza kuwa mwili wa mwalimu huyo ulipatikana usiku wa jana nyuma ya nyumba yake, dakika chache baada ya kutoka shuleni alikokuwa akisimamia masomo ya ziada.

 "Mimi pamoja na maafisa wetu wa polisi tulifahamishwa jana usiku kuwa kuna mwalimu amewaua katika shuel ya upili  ya Hopewell. Tulifika hapa na kweli tukapata mwili wa mwalimu ukiwa chini, ikiwa dhahiri kwamba amepasuliwa kichwa kwa kupigwa kitu kizito,'' amesema chifu Kering na kuongeza kuwa maafisa wamemkamata mwanafunzi mmoja kutoka shule hiyo na mwingine kutoka shule jirani ambao wanasaidia kwa uchunguzi. 

''Kama serikali tutafanya uchunguzi na tuone kwamba waliohusika wametiwa nguvuni na kushtakiwa.” Ameahidi chifu afisa huyo.

Wahalifu waigeuza shule uchochoro wao

Kenia Schüler in Nakuru trauern um den Tod ihres Lehrers
Watu walikuwasanyika kufuatilia kwa karibu kisa hichoPicha: DW/W. Mbogho

Eneo palipo shule hiyo pamehusishwa na uhalifu mwingi ambapo dawa za kulevya, vileo na simu za mkononi kati ya vitu vingine vimesemekana kuingizwa shuleni humo kwa njia isiyo halali. Vitalis Kahenda, mkurugenzi wa shule hiyo ya upili ya Hopewell anaieleza hii kama changamoto kubwa inayowakabili. "Tuna wanafunzi zaidi ya 400, wavulana kwa wasichana ingawa huduma za bweni ni za wasichana pekee. Swala la uhalifu katika eneo hili ni kero kubwa na limeathiri shule yetu pakubwa.'' Amelalamika Kahenda.

Mkuu huyo wa shule amesema pia kwamba wamelalamika mara kadhaa kwa maafisa wa usalama hasa kuwahusu hao watu wawili ambao walionekana shuleni hapo. ''Sio vileo pekee, hata dawa za kulevya huuziwa wanafunzi wetu, lakini hakuna lolote lililofanywa na maafisa hao. Hatuna udhibiti wa mambo lakini maafisa wa usalama wana kazi kubwa ya kufanya.” amemalizia.

Wanafunzi wamlilia mwalimu wao

Tukio hili limeibua hali ya majonzi na wasiwasi katika shule hiyo, wanafunzi wakionekana kumuomboleza mwalimu waliyemtaja kama mwalimu mwenye bidii. Faiza Otunga, mmoja wa wanafunzi anakumbuka matukio ya jana usiku, "mwalimu wetu alikuwa akitembelea kila darasa kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne. aliwazungumzia wanafunzi kwa upole. Huwa anatupa ushauri mzuri sana.”

Kenia Schüler in Nakuru trauern um den Tod ihres Lehrers
Lango la kuingia katika shule ya sekondari ya HopewellPicha: DW/W. Mbogho

Mwingine, Alvin Ochieng amesema ameshtushwa sana na kifo cha mwalimu wake, "ni kwa huzuni kubwa tunamuomboleza mwalimu Peter Omari, aliyekuwa mwalimu wetu wa somo la Fizikia na Kompyuta. Tulimpenda sana hata siwezi kuelezea.”

Mke wa mwalimu huyo ni mlezi katika shule hiyo na alikuwa amewachwa nyuma kuhakikisha kuwa wanafunzi wote walio kwenye mabweni wamelala bila kufahamu kuwa wahalifu hao walikuwa wanamsubiri mme wake kando ya nyumba yao ilioko karibu na shule hiyo.

Mamake marehemu, Florence Kerubo amesema amempoteza mtoto wa kwanza wa kiume aliyekuwa mwaminifu na mwenye upenzo mwingi. "Nimetumia pesa nyingi kumsomesha Peter na nilikuwa na matumani makubwa kwake. Wakati alipata kazi hapa akaendelea kuifanya alijiunga na chuo kikuu cha Mt. Kenya, sahii alikuwa mkufunzi alikuwa amalizie mwezi wanne, sssa ndoto yake imeishia hapo.'' amesema kwa majonzi mama huyo, na kuiomba serikali kufanya uchunguzi wa kina ijulikane sababu ya mtoto wake kuuawa.

Mwili wa Peter umehifadhiwa katika chumba cha maiti cha hospitali kuu ya kaunti ya Nakuru huku washukiwa watatu akiwemo mwanafunzi wakizuiliwa katika kituo cha polisi mjini Nakuru.

Mwandishi: Wakio Mbogho/DW Nakuru

Mhariri: Daniel Gakuba