Mvutano India na Pakistan waongezeka | Matukio ya Kisiasa | DW | 30.09.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Kashmir

Mvutano India na Pakistan waongezeka

Viongozi wa Pakistan na India wanashiriki mikutano kutathmini usalama katika mpaka kati ya nchi zao. Mikutano hiyo inafanyika wakati ambapo majeshi ya pande zote mbili yako katika hali ya tahadhari.

India na Pakistan zimewahi kupigana mara mbili kuhusu jimbo hilo la Kashmir, huku kila upande ukidhibiti sehemu ya jimbo hilo. India imechukua hatua ya mapema  kwa  kuwaondoa wanakijiji wake zaidi ya elfu 10 wanaoishi karibu na mpaka wa Pakistan. Waziri mkuu Narendra Modi aliviagiza  vyombo vya usalama kuimarisha doria katika majimbo ya Jammu na Kashmir ambayo ni sehemu ya kilomita elfu 3,300 ya mpaka kati ya mataifa hayo jirani yenye uwezo mkubwa wa zana za kinuklia. India ilichukua hatua hiyo ya kuwahamisha raia wake  baada ya kutangaza kufanya  mashambulizi katika eneo la mpaka la kashmir linaloshikiliwa na Pakistan, dhidi ya wapiganaji  wanaoshukiwa walikuwa wakijitayarisha  kutekeleza mashambulizi nchini India.

Pakistan yashtumu mashambulizi ya India

Hata hivyo serikali ya Pakistan kupitia  waziri wake wa maswala ya kigeni  Mohammed Zakaria imeyalaani mashambulizi hayo na India. "Katika muda wa siku 83 zilizopita.Majeshi ya India yamewaua  zaidi ya wakashimir waislamu wasiokuwa na hatia 100 wakiwemo watoto, akinamama na vijana. Pia yamewajeruhi macho zaidi ya watu 800 kwa kutumia bunduki marisao, mamia kupofuka kabisa na wengine kuwa na uwezo wa kuona kidogo. Zaidi ya watu elfu 12 pia wamejeruhiwa," alisema waziri huyo.

Wanaopinga mauaji ya hivi karibuni jimboni Kashmir (Reuters/D.Ismail )

Wanaopinga mauaji ya hivi karibuni jimboni Kashmir

Mzozo kati ya Pakistan na India umeendelea kwa miaka mingi ambapo mara kwa mara wamekuwa wakishambuliana. Balozi wa Pakistan katika umoja wa mataifa Maleeha Lodhi amesema  taifa lake linautaka umoja wa mataifa kuingilia kati mgogoro wa sasa ili kutuliza hali.

Mwanajeshi wa India atekwa

Taarifa nyingine ni kuwa majeshi ya Pakistan yametangaza kumteka mwanajeshi wa India  ambae alivuka mpaka unaodhibitiwa na mataifa hayo mawili, saa chache baada ya wanajeshi hao kushambuliana kwa risasi.

Hata hivyo India imesema mwanajeshi huyo alivuka eneo hilo bila kukusudia na atarejea nyumbani baada ya mashauri ya kijeshi.Taharuki kati ya majirani hao ilizuka mapema mwezi huu baada ya wapiganaji kuvamia kambi ya majeshi ya India eneo la Kashmiri na kuwaua 19 miongoni mwao. New Delhi inadai wapiganaji hao  wanaendesha shughuli zao nchini Pakistan.

Mara zote India imekuwa ikipinga vikali maazimio yanayotolewa na Umoja wa Mataifa yanayotaja kwamba Kashmir ni sehemu ya Pakistan. Mgogoro wa Kashmiri ulianza mwaka 1947 wakati wa kugawanywa Bara Hindi. Pakistan inaamini, Umoja wa Mataifa una wajibu wa kuheshimu maazimio yake na kuilazimisha India nayo iheshimu maazimio hayo hususan suala  la kupewa haki wananchi Waislamu wa Kashmiri ya kujiamulia wenyewe mustakbali wao.

Mwandishi: Jane Nyingi/RTRE/DPAE

Mhariri: Yusuf Saumu

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com