1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Muongozo wa kutekeleza makubaliano ya Paris wafikiwa

Caro Robi
16 Desemba 2018

Takriban mataifa 200 yamefikia makubaliano yatakayopiga jeki mkataba wa Paris uliofikiwa mwaka 2015 kwa lengo la kudhibiti ongezeko la joto duniani ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

https://p.dw.com/p/3ACcV
Polen, COP24-Präsident Michal Kurtyka während einer Abschlusssitzung der COP24-Klimakonferenz 2018 in Katowice
Picha: Reuters/K. Rempel

Wajumbe kutoka matiafa hayo karibu 200 ambao wamekuwa wakijadiliana kwa wiki mbili mjini Katowice nchini Poland, hatimaye wamefikia muongozo madhubuti utakaohakikisha kuwa malengo ya mkataba wa Paris wa kupunguza joto ulimwenguni hadi chini ya nyuzi mbili yanatimizwa.

Rais wa mkutano huo kuhusu mabadiliko ya tabianchi COP24 Michal Kurtyka amesema kuweka pamoja mpango wa kutekeleza makubaliano ya Paris ni wajibu mkubwa, akiongeza kuwa ilikuwa njia ndefu kufikiwa muafaka katika mkutano wa Katowice.

Hatua za dharura zinahitajika

Miongoni mwa yaliyoafikiwa ni pamoja na namna gani nchi zitatoa ripoti kuhusu kiwango cha gesi chafu katika mataifa yao na juhudi za kuipunguza, hakikisho la ufadhili wa kifedha kwa mataifa maskini ili kusaidia kupunguza gesi ya Carbon, kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi yasiyoepukika pamoja na kulipa kwa ajili ya uharibifu ambao tayari umetokea.

UN-Klimakonferenz 2018 in Katowice, Polen | Gruppenbild
Viongozi wa nchi mbalimbali na wa asasi za Umoja wa Mataifa katika mkutano wa COP24Picha: picture-alliance/dpa/Keystone/P. Klaunzer

Lakini nchi zinazokumbwa na athari kubwa za kimazingira kama mafuriko, ukame na athari nyingine kali zilizotokana na mabadiliko ya hali ya hewa zimesema makubaliano hayo yaliyofikiwa Katowice yanakosa malengo madhubuti kuhusu namna ya kupunguza gesi chafu, hadi kiwango kinachohitajika.

Balozi wa Misri Wael Aboulmagd aliyewakilisha kundi la nchi zinazoendelea G77 ikiwemo China amesema muongozo huo wa kuyatekeleza malengo ya mkataba wa Paris haujashughulikia mahitaji ya dharura ya nchi zinazoendelea ambazo zimewekwa katika kile alichokitaja tabaka la pili.

Mkurugenzi mkuu wa Greenpeace Jennifer Morgan amesema wanazidi kushuhudia migawanyiko isiyohitajika kati ya mataifa yaliyo katika hatari ya visiwani na nchi masikini zikiwa upande mmoja na nchi tajiri ambazo zinaweza kuzuia hatua kuchukuliwa kuhusu tabianchi au kufeli kuwajibika kwa kutochukua hatua za haraka kuyaokoa mazingira.

Nchi zinazoendelea zilitaka ufafanuzi zaidi kutoka kwa nchi tajiri kuhusu mustakabali wa siku za usoni wa kudhibiti athari za mabadiliko ya tabia nchi kwa kueleza bayana ufadhili utatoka wapi na ni hatua gani hasa zitachukuliwa kuchukua hatua za kuepusha maafa zaidi.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema Ufaransa na Ulaya zinahitaji kuonesha njia huku akisifu hatua zilizopigwa katika mazungumzo hayo ya Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi.

Kupitia ukurasa wa Twitter, Macron amesema jumuiya ya kimataifa bado inajitolea kuhakikisha vita dhidi ya athari za mabadiliko ya hali ya hewa vinashinda.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema mapambano hayo ya kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi ni mwanzo tu.

Mwandishi: Caro Robi/Afp/dpa

Mhariri: Sylvia Mwehozi