Muammar Gaddafi amefariki dunia
21 Oktoba 2011Akitangaza kifo hicho katika mji mkuu wa Libya Tripoli, Jibril amesema, wameungojea wakati huo wa kihistoria kwa muda mrefu. Sasa umewadia wakati wa kuwa na Libya mpya, Libya iliyoungana. Hapo awali, kamanda wa serikali mpya ya Libya alitangaza kuwa Gaddafi alijeruhiwa katika mapambano ya kuuteka mji wa Sirte, alikozaliwa kiongozi huyo wa zamani. Muda mfupi baadae alifariki kutokana na majeraha yake. Maiti yake imepelekwa katika msikiti mmoja mjini Misrata.
Inasemekana kuwa kiongozi huyo wa zamani wa Libya alikamatwa alipokuwa akikimbia kutoka mji wa Sirte katika mlolongo wa magari. Gaddafi anatazamiwa kuzikwa kwa siri baadae leo hii. Kwa mujibu wa ripoti za televisheni ya Libya, hata wanae wawili wa kiume, Saif al-Islam na Mutassim wameuawa. Maiti zao zimepelekwa hospitali mjini Sirte.
Mji huo wa pwani ulikuwa ngome ya mwisho ya Gaddafi na ulidhibitiwa na wafuasi wake mpaka dakika ya mwisho.Kifo cha kiongozi huyo wa zamani, kimeondoa kizingiti kilichokuwepo kwa serikali mpya ya mpito, miezi miwili baada ya waasi waliosaidiwa na nchi za magharibi kuuangusha utawala wa Gaddafi wa miaka 42 kwa kuuteka mji mkuu Tripoli.
Nae Rais wa Marekani Barack Obama mjini Washington amesema, kifo cha Muammar Gaddafi kimefunga ukurasa mrefu wa maumivu kwa watu wa Libya. Akithibitisha kifo cha Gaddafi, Rais Obama alisema, hatimae utawala wa mabavu humalizika. Akasisitiza mchango uliotolewa na Walibya kumuangusha Muammar Gaddafi. Amesema, sasa watu wa Libya wenyewe, wanaweza kujiamulia mustakabali wa nchi yao.
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema, hatimae njia ipo wazi kwa mchakato wa amani wa kisiasa. Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa jumuiya ya kujihami NATO, Jemadari Anders Fogh Rasmussen amesema, sasa operesheni ya Libya itasitishwa kwani utawala wa Muammar Gaddafi umemalizika. Hata hivyo amesema, operesheni hiyo itasitishwa baada ya kushauriana na Umoja wa Mataifa na Baraza la Mpito la Libya.
Shirika la habari la Ujerumani, DPA limewanukulu mabalozi wakisema kuwa Ijumaa ya leo, mabalozi wa nchi wanachama wa NATO watakuwa na mkutano wa dharura kuujadili mpango wa kumaliza operesheni za kijeshi nchini Libya. Lakini Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, William Hague mjini London, amesema, isifanywe haraka kuondoka na amekataa kupanga tarehe ya kuimaliza operesheni hiyo nchini Libya. Akaongezea kuwa operesheni hiyo ya NATO, itamalizika pale Baraza la Mpito la Libya litakapotaka.
Baadae leo hii, Rais wa serikali ya mpito ya Libya, Mustafa Abdel Jalil, anatazamiwa kutangaza rasmi kukombolewa kwa nchi hiyo kutoka utawala wa Gaddafi.