1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mtazamo mpya unahitajiwa kupiga vita njaa duniani

16 Novemba 2009

Mkutano wa kilele unaohusika na njaa duniani unastahili kusifiwa- lakini siasa zinangángánia miradi ya kuimarisha hali ya uchumi na hivyo huzuia suluhisho endelevu.

https://p.dw.com/p/KYXM
Jacques Diouf, Director-General of United Nations Food and Agriculture Organization FAO, seen, during a press conference held at the FAO headquarters, in Rome, Sunday, Nov. 15, 2009, ahead of a World Summit on Food Security which opens in Rome Monday, Nov. 16 for three days. (AP Photo/Pier Paolo Cito)
Jacques Diouf, Mkurugenzi Mkuu wa FAO - Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa.Picha: AP

Marais,viongozi wa serikali na wajumbe waandamizi wanakutana mjini Roma Italia kuanzia leo hadi Jumatano ijayo kufuatia mualiko uliotolewa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa FAO. Viongozi hao wanajadili mzozo wa chakula unaokabiliwa duniani.

Mtu ahitaji kufanya utafiti mrefu ili kuweza kutambua kuwa njaa na umasikini ni mambo yanayokwenda sambasamba. Asilimia 70 ya umma unaoishi katika hali ya umasikini mkubwa hukutikana katika maeneo ya mashambani. Ikiwa mkulima anaetazamiwa kutulisha sote, hushindwa kujilisha mwenyewe, basi hapo bila shaka kuna kitu kisicho sahihi hata kidogo.

Ni jambo lisiloeleweka kwanini imechukua muda huu wote kutambua kuwa vita dhidi ya njaa na umasikini vitaweza tu kuleta natija ikiwa fedha zitatumiwa kuendeleza maeneo ya mashambani. Sasa ndio mkutano wa FAO mjini Roma unataka kuhimiza uwekezaji utakaosaidia kuleta maendeleo katika maeneo ya mashambani.

Kabla ya mkutano huo,Mkurugenzi Mkuu wa FAO Jaques Diouf alipendekeza watu wafunge kwa saa 24 kama ishara ya mshikamano kwa watu bilioni moja wanaosumbuliwa na njaa duniani. Hata ikiwa kuna watu watakaofunga kwa saa 24,hiyo haitosaidia. Kwani kinachohitajika kupiga vita njaa na umasikini kwa ufanisi, ni mtazamo mpya kote duniani. Na hapo si kuhusu chakula tu, kwani ili kuweza kuleta mabadiliko ya maana, hata masuala ya mazingira,uchumi na fedha yanapaswa kuzingatiwa kwa msingi endelevu na sio kuhimiza matumizi.

Serikali mpya ya Ujerumani inataka kuchochea ukuaji wa kiuchumi kwa kuwahimiza wananchi kununua zaidi. Je, kupalilia kiu cha kununua vitu ni njia ya kupambana na mgogoro wa kiuchumi?au kuongeza matumizi kama njia ya kupiga vita njaa? Hayo yote hayatosaidia kitu - haitosaidia katika kukabiliana na mzozo wa chakula,mzozo wa fedha wala matatizo ya mazingira. Mtu anaweza kusema atakacho, lakini wenye kununua ni wale wenye pesa na wanaoumia ni wale walio masikini.

Mwandishi:H.Jeppesen/ZPR/ P.Martin

Mhariri: Sekione Kitojo