Mpasuko ndani ya Labour ya Uingereza | Matukio ya Kisiasa | DW | 18.02.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

BREXIT

Mpasuko ndani ya Labour ya Uingereza

Wabunge saba wa chama cha Labour wamejiuzulu wakipinga kile wanachokiita muelekeo wa chama hicho kwa Brexit na hisia za chuki dhidi ya Wayahudi, hali inayoashiria mpasuko mkubwa wa kisiasa kwenye historia ya Labour.

Wakizungumza na waandishi wa habari mapema leo (Jumatatu 19 Februari)  jijini London, wabunge hao saba mashuhuri walisema sasa wataunda kundi linalojitegema ndani ya bunge kupingana na mtazamo wa sasa wa chama chao cha zamani.

Mmoja wao, Luciana Berger, aliulaumu uongozi wa juu wa chama hicho kwa kuyaacha maadili ambayo yalimfanya ajiunge nacho miaka ishirini iliyopita, wakati wakiwa mwanafunzi:

"Sasa maadili haya yamekuwa yakivunjwa, kuhujumiwa na kushambuliwa kila mara. Kwa kuwa chama cha Labour sasa kinakataa kuweka maslahi ya wapigakura na nchi yetu mbele ya maslahi ya chama. Siwezi kubakia kwenye chama, ambacho nimefikia kwenye hitimisho la kusikitisha kwamba kina chuki dhidi ya Wayahudi ndani yake;" alisema mbunge huyo. 

Hofu ya mpasuko ndani ya chama cha Labour imekuwa kwa kipindi kirefu, huku maoni yakipingana kuhusu uongozi wa Jeremy Corbyn.

Wengi wanamtuhumu mnadhimu huyo wa upinzani bungeni kwa kukosa imani na Umoja wa Ulaya, wakisema anashindwa kuchukuwa msimamo wa wazi juu ya suala la Uingereza kujitoa kwenye Umoja huo kwa muda mrefu.

Hata hivyo, mwenyewe Corbyn alisema anafadhaishwa na uamuzi wa wabunge walioshindwa kuzifanyia kazi sera zilizowavutia wapigakura kwa mamilioni kwenye uchaguzi wa 2017.

Wakusudia kuunda chama kipya

Mbali na Luciana Berger, wabunge wengine walioiwacha Labour leo hii ni pamoja na Chris Leslie, Angela Smith, Gavin Shuker, Mike Gapes, Ann Coffey na Chuka Umunna.

Labour Partei Mitglieder verlassen Partei Großbritannien (Reuters/S. Dawson)

Mbunge Chuka Umunna, mmoja wa waliokiwacha mkono chama cha Labour.

Kujiuzulu kwa Umunna kulitajwa na wachambuzi wa siasa za Uingereza kuwa ni pigo zaidi kwa chama hicho, kwani ni yeye ndiye anayeongoza kundi linalotaka kura nyengine ya maoni juu ya Brexit na kwa wengi anachukuliwa kama nyota mpya ya Labour.

Mbunge huyo mwenye asili ya Afrika aliuita uamuzi wake wa kuachana na Labour kuwa ni mgumu hata kwake mwenyewe, lakini ni akawaalika Waingereza kuwaunga mkono kuunda chama kipya.

"Unaweza kutokea kwenye mizizi ya Labour au imani nyengine za kisiasa na bado huu ukabakia kuwa uamuzi mgumu sana, lakini fikiria moja tu: hupaswi kujiunga na chama cha kisiasa kisha ukatumia miaka na miaka kupambana na waliomo ndani yake. Unajihusisha na siasa, unajiunga na chama, kuubadili ulimwengu. Hivyo tunawaalikeni kuacha vyama vyenu na kutusaidia kuunda maridhiano mapya ya kuipeleka Uingereza mbele," alisema Umunna.

Kujiuzulu kwa wabunge hao kunakuja pia katika wakati ambao polisi inasema imeanza uchunguzi juu ya tuhuma za kuwepo kauli za chuki dhidi ya Wayahudi kutoka kwa wanachama wa Labour.

Tuhuma za aina hiyo zimekuwa zikitolewa mara kwa mara hata dhidi ya Corbyn mwenyewe, ambaye mwaka jana alikiri kwenye picha ya vidio kwamba kesi dhidi ya kauli hizo kwa wanachama wake zimekuwa zikiendeshwa kwa kasi ndogo. 

Mwandishi: Mohammed Khelef/AP/dpa
Mhariri: Daniel Gakuba

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com