1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Modeste Bahati ndiye spika mpya wa seneti DRC

3 Machi 2021

Baraza la Seneti Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limemchagua Modeste Bahati Lukwebo kuwa spika wake kuchukua nafasi ya Alexis Thambwe Mwamba.

https://p.dw.com/p/3q8tl
Demokratischen Republik Kongo | Modeste Bahati Lukuebo legt dem Präsidenten Félix Tshisekedit einen Bericht vor
Picha: Giscard Kusema

Mwamba alijiuzulu mwezi uliopita kutokana na shinikizo kutoka kwa maseneta.

Bahati Lukwebo ni mshirika wa zamani wa rais mstaafu Joseph Kabila ambaye alitengana naye kutokana na kutopata nafasi hii ya spika wa Baraza la Seneti.

Baada ya kuvunjika kwa muungano kati ya Kabila na Rais Felix Tshisekedi, Lukwebo alijiunga na Umoja wa Taifa wa Rais Tshisekedi na kumhudumia kwa utafiti ili kubaini wingi bungeni. Maseneta 98 ​​walipiga kura zao katika uchaguzi wa jana Jumanne.

Kamati ya dharura ndiyo iliyosimamia uchaguzi huo wa spika

Lukwebo alikuwa mgombea pekee kwenyi nafasi ya Spika na alipata kura 89, hivyo kachaguliwa kuwa spika mpya wa Baraza la Seneti.

Uchaguzi huo wa Sekretarieti ya Seneti uliandaliwa na kusimamiwa na kamati ya dharura chini ya uongozi wa Leon Mamboleo ambaye alithibitisha matokeo kama ifuatavyo.

Senat in Kinshasa, Demokratische Republik Kongo
Bunge la seneti jamhuri ya Kidemokrasia ya CongoPicha: AFP/Getty Images/J. D. Kannah

''Seneta Bahati Lukwebo Modeste alipata kura 89 kati ya kura nyingi zilizopigwa katika duru ya kwanza. Na hivyo, anachaguliwa kama Spika wa Seneti. Kwa niaba ya Bunge la Baraza nampongeza kwa dhati,'' alisema Mamboleo.

Bahati Lukwebo ambae ni kiongozi wa chama AFDC siye mgeni katika siasa za Kongo, kwani aliwahi kuwa waziri mara mbili chini ya utawala wa rais wa zamani Joseph Kabila ambaye alikuwa mshirika wake, ingawa walitengana wakati ambapo Kabila hakumruhusu kuchukuwa wadhifa wa Spika wa Baraza la Seneti.

''Maseneta kwa kuamua kunichagua kwa wingi, waligundua kuwa nina kitu cha kuchangia katika ujenzi wa taifa, kwa sababu, kama unavyojua, lazima tuirejeshe picha bora ya Seneti. Lazima tuwe katika utawala bora kama ilivyoainishwa na mkuu wa mchi, Rais Félix Tshisekedi,'' alisema Lukwebo.

Bahati anatarajiwa kutimiza alichoahidi wakati wa kampeni

Lakini kwa kweli, ni kipi kinachotarajiwa toka kwake Bahati Lukwebo kama spika mpya wa Baraza la Seneti? Profesa Nkere Tanda kutoka Chuo Kikuu cha Kinshasa anajibu.

Mpasuko katika muungano wa FCC Congo

''Tunachokitarajia huenda pamoja na kile alichoahidi wakati wa kampeni yake. Yaani kuhakikisha kwamba chumba hiki kinafanya kazi kwa mahitaji ya raia, kwa sababu kama unavyojua, maseneta wanawakilisha mikoa, hiyo inamaanisha kuwa wanazungumza kwa niaba ya raia. Halafu watalazimika kuyazingatia hayo,'' alisema Profesa Tanda.

Ofisi ya Seneti inawajumuisha wajumbe saba, lakini ni sita tu waliochaguliwa jana Jumanne, kwani Waziri Mkuu wa zamani Samy Badibanga ambae ni makamu wa kwanza wa spika, ndiye alinusurika toka ofisi ya Thambwe Mwamba.