Mnorway atuhumiwa kupanga uvamizi wa Westgate | Matukio ya Afrika | DW | 18.10.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Mnorway atuhumiwa kupanga uvamizi wa Westgate

Raia wa Norway mwenye nasaba ya kisomali anashukiwa kuwa miongoni mwa washambuliaji waliolivamia jengo la maduka la Westgate mjini Nairobi, Kenya, (21.09.2013) uliopita ambapo watu 67 waliuwawa.

Smoke rises over Westgate shopping centre after an explosion in Nairobi, September 23, 2013. Powerful explosions sent thick smoke billowing from the Nairobi mall where militants from Somalia's al Qaeda-linked al Shabaab group threatened to kill hostages on the third day of a raid in which at least 59 have already died. REUTERS/Karel Prinsloo (KENYA - Tags: CIVIL UNREST CRIME LAW) ***FREI FÜR SOCIAL MEDIA***

Moshi ukifuka kutoka jengo la maduka la Westgate

Shirika la BBC limeripoti kwamba Hassan Abdi Dhuhulow, kijana wa umri wa miaka 23, anatuhumiwa kusaidia kupanga na kutekeleza shambulizi dhidi ya jengo la maduka la Westgate Septemba 21 mwaka huu. Kijana huyo alizaliwa nchini Somalia, lakini yeye na familia yake wakahamia nchini Norway kama wakimbizi mnamo mwaka 1999. Hayo ni kwa mujibu wa jamaa wa familia hiyo waliozungumza na BBC kutoka mji wa Larvik, yapata kilometa 120 kusini mwa mji mkuu wa Norway, Oslo. Shirika hilo lilimnukuu jirani wa familia ya Hassan, Morten Henriksen, aliyetoa maelezo kumhusu kijana huyo.

"Alikuwa kijana mwenye hasira, hakupenda maisha nchini Norway. Alijikuta kwenye matatizo na vita na babake alikuwa na wasiwasi," amesema Henriksen wakati alipozungumza na BBC. Wiki iliyopita shirika la ujasusi la Norway, PST, lilisema lilikuwa limeanzisha uchunguzi baada ya kupata taarifa kuhusu uwezekenao wa raia wa Norway mwenye asili ya Kisomali kuhusika katika kuratibu na kufanya shambulizi dhidi ya jengo la maduka la Westgate. Shirika hilo pia limesema wachunguzi wa Norway wametumwa mjini Nairobi kushirikiana na wenzao wa Kenya.

A man only identified by his first name, Stephen (C) is comforted by Pastor Elizabeth Akinyi (R) and family members at the city mortuary in Nairobi on September 23, 2013. Stephen's father was killed in the Westgate mall siege on September 21, 2013. Kenyan Defence troops remain inside the mall, in a standoff with Somali militants after they laid siege to the shopping centre shooting and throwing grenades as they entered. AFP PHOTO/Carl de Souza (Photo credit should read CARL DE SOUZA/AFP/Getty Images)

Jamaa wakiwalilia wapendwa wao waliokufa Westgate

Mashihidi waliokuwa ndani ya jengo la Westgate walieleza jinsi wapiganaji walivyoingia mida ya alasiri siku ya Jumamosi Septemba 21, wakati lilipokuwa limejaa wateja, na kuanza kuwafyetua risasi kiholela na kuwarushia maguruneti watu waliokuwa wamekwenda kununua vitu pamoja na wafanyakazi wa maduka ya jengo hilo.

Serikali ya Kenya ilitangaza kumalizika kwa uvamizi huo baada ya siku nne. Polisi ya nchi hiyo iliwataja washambuliaji wanne kuwa Abu Baraa Al Sudani, Khatab Ali Khane na mwanamume mmoja aliyetambulishwa kwa jina moja la Umayr - wote Wasomali, pamoja na Mkenya mmoja mwenye nasaba ya Kisomali, Omar Nabhan.

Wataalamu waonya kuhusu al Shabaab

Wakati haya yakiarifiwa, wataalamu wa masuala ya usalama wameonya juu ya kuwepo kitisho kikubwa cha vikundi vya wapiganaji wa al Shabaab na ongezeko la wafuasi wa kundi hilo. "Kama bado hamjajifunza kutokana na mkasa wa Westgate, mashambulizi mengine mengi yanakuja," lilisema bango moja lililotundikwa kwenye mikutano ya hadhara katika mji wa bandari wa Barawe, kusini mwa Somalia wiki hii, ambao ni ngome ya al Shabaab. "Kwa kila muislamu atakayeuwawa Kismayo, Kenya italipa gharama ya mauaji hayo," likasema bango lengine, likizungumzia mji huo uliotekwa mwaka jana na wanajeshi wa Kenya walioko Somalia.

Mtaalamu wa masuala ya usalama, Richard Dowden, Mkuu wa shirika la Royal African Society la Uingereza, ameonya shambulizi la Wesgate linapendekeza makamando wa kundi la al Shabaab wamehama kutoka siasa za ndani ya Somalia na kuikaribia ajenga ya kimataifa ya mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda. Kundi la al Shabaab linaendelea kuwasajili vijana katika eneo la Afrika Mashariki. EJ Hagendoorn wa shirika la kimataifa linaloshughulikia mizozo, ICG, amesema kundi hilo hutumia kisasi, uzalendo na kujitenga kama mbinu za usajili. Alisema hatua ya kundi hilo kukiri hadharani kuhusika na shambulizi la Westgate ililenga kuchochea uhasama dhidi ya wasomali na waislamu nchini Kenya na kusini mwa Somalia.

Mwandishi: Josephat Charo/AFPE

Mhariri: Saumu Mwasimba