Mkutano wa kilele wa AU wamalizika | Matukio ya Afrika | DW | 10.02.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Mkutano wa kilele wa AU wamalizika

Wakuu wa mataifa ya Afrika wamekutana mwishoni mwa wiki hii mjini Addis Ababa Ethiopia kwa ajili ya mkutano wa kila mwaka wa kilele, huku wametoleana mwito wa kusuluhisha mizozo ya ndani na kuzuia uingiliaji kutoka nje. 

Wakuu wa mataifa ya Afrika wamekutana mwishoni mwa wiki hii mjini Addis Ababa, Ethiopia kwa ajili ya mkutano wa kila mwaka wa kilele uliokuwa na maudhui inayosema "kunyamazisha milio ya risasi: Imarisha uwezo wa Afrika kuelekea maendeleo", huku wakitoleana mwito kwa wao wenyewe kuchukua hatua katika kusuluhisha mizozo ya ndani ili kuzuia uingiliaji kutoka nje. 

Afrika kusini imechukua uenyekiti wa Umoja huo kwa mwaka huu wa 2020, kutoka kwa Misri. Rais Cyril Ramaphosaalinukuliwa akisema Afrika Kusini itakuwa mwenyeji wa mkutano wa kilele wa mwezi Mei utakaojadili pamoja na masuala mengine changamoto dhidi ya amani na usalama wa bara la Afrika.

Ramaphosa alisema "Mkutano tutakaouandaa utatakiwa kufikiria hatua madhubuti ambazo sisi kama waafrika tunatakiwa kuzichukua ili kumaliza mizozo na vitendo vya ugaidi vinavyojitokeza kwenye mataifa na kanda mbali mbali kama za Sahel, ambavyo kwa sasa vinasambaa kwenye maeneo mengine ya Kusini mwa Afrika pia."

Äthiopien AU-Gipfel in Addis Abeba | Cyrial Ramaphosa übernimmt Vorsitz von Abdel Fattah al-Sisi

Afrika Kusini imepokea uenyekiti wa Umoja huo na kuahidi kuitisha mkutano mwingine wa kilele ifikapo mwezi Mei.

Mizozo ya Sudan Kusini, Jamhuri ya Afrika ya Kati, mali na ukanda wa Sahel ni miongoni mwa ile iliyopewa kipaumbele kwenye majadiliano ya mkutano huo wa kilele wa Umoja huo wa Afrika. Rais Ramaphosa alisisitiza kwamba Afrika inatakiwa kuchukua nafasi yake katika kusuluhisha mizozo yake ya ndani ili kuzuia uingiliaji wa nje.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ambaye pia ameshiriki katika mkutano huo wa kilele pamoja na masuala mengine amewaeleza wakuu hao kwamba bara la Afrika linatakiwa kujiimarisha katika kukabiliana na athari mbaya za mabadiliko ya hali ya hewa ambazo tayari ziko dhahiri.

"Joto linaongezeka mara mbili ya wastani wa kidunia. Mwaka jana hali ilikuwa mbaya sana. Pamoja na athari za vimbunga Idai na Keness, taarifa zinasema kwamba vilitokana na mabadiliko ya tabianchi, kuanzia Sahel hadi Zambia, Kenya hadi Madagascar" alisema Guterres.

Viongozi hao pia wamejipa changamoto ya kujikita zaidi katika kuwawezesha wanawake na wasichana. Katika kutekeleza hilo, tayari Umoja huo pamoja na tume ya kiuchumi ya Umoja wa Mataifa kwa Afrika wamezindua wakfu wa kuwasaidia wanawake kupata mikopo kwa ajili ya biashara. Wakfu huo wa masuala ya Wanawake na uongozi utakuwa na kiasi cha dola bilioni moja kama mtaji ama uwekezaji.