1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Misri yapeleka mzozo wake na Ethiopia baraza la Usalama

Sekione Kitojo
20 Juni 2020

Misri imesema leo Jumamosi (20.06.2020) imeliomba baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuingilia kati mzozo wake wa muda mrefu na Ethiopia kuhusu bwawa la umeme katika mto Nile.

https://p.dw.com/p/3e58Q
Äthiopien Luftbild Grand-Ethiopian-Renaissance-Talsperre
Picha: DW/Negassa Desalegen

Misri inahofu kwamba bwawa hilo litapunguza kiasi cha maji inachohitaji kwa ajili  ya  shughuli  muhimu  katika  nchi hiyo.

Hatua ya  Misri inakuja siku chache baada ya  duru ya mazungumzo kati ya Misri, Ethiopia na Sudan  kuhusiana  na  bwawa  hilo kumalizika  bila  ya kupatikana  muafaka. Addis Ababa inatarajia kuanza  kulijaza bwawa hilo  la Grand Ethiopian Renaissance Dam (GERD) mwezi ujao.

Äthiopien Addis Abeba | Report | Grand Ethiopian Renaissance Dam
Bwawa linalojengwa na Ethiopia la Grand Renaissance Dam Picha: DW/N. Desalegen

Wizara ya mambo ya kigeni  ya  Ethiopia  imesema  katika  taarifa siku  ya  Jumamosi  kuwa  ombi  la  Misri  linalitaka  baraza  la Usalama  kuingilia  kati  ili kuhakikisha  mazungumzo "kwa nia njema" baina ya  nchi  hizo tatu za  mto Nile.

Misri "ilichukua  hatua  hii kutokana  na  kushindwa  kwa mazungumzo ya  hivi  karibuni kuhusiana  na  bwawa  hilo kutokana na  msimamo  hasi  wa  Ethiopia  ambao  unakuja  katika mfumo  wa kuchukua  hatua katika  msimamo  ule  ule katika  muda  wa  muongo mmoja uliopita wa majadiliano hayo  magumu," wizara  hiyo  imesema katika  taarifa.

Lawaam kwa Ethiopia

Misri inailaumu  Ethiopia  kwa mkwamo  huo , ikisema  inakosa "nia njema ya kisiasa" kufikia  makubaliano  ya  mwisho katika  mzozo huo.

BG Grand Renaissance Dam | Der äthiopische Premierminister Abiy Ahmed Ali mit dem ägyptischen Präsident Abdel-Fattah al-Sisi (2018)
Rais wa Misri Abdel-Fattah al-Sisi akizungumza na waziri mkuu wa Ethiopia Abiy AhmedPicha: Imago Images/Xinhua

Ethiopia ilianza ujenzi wa  bwawa  hilo litakalozalisha  umeme  lenye thamani  ya  dola  bilioni 4.8 mwaka  2010, kama  sehemu ya mpango  wa  kupanua  uuzaji  wake  wa  nishati nje  ya  nchi.

Misri inategemea  kwa  kiasi  kikubwa  maji  ya  mto  Nile  kwa kilimo, viwanda  na  matumizi  ya  nyumbani  ya  maji na  inahofia kuwa  bwawa  hilo litaathiri upatikanaji  wa  maji  katika  nchi  hiyo. Ethiopia inasema  hofu ya  Misri haina  msingi.