Migomo yaanza kuleta athari Ufaransa
16 Oktoba 2010Ufaransa inakabiliwa na ishara za kwanza za uhaba wa mafuta wakati migomo dhidi ya mageuzi ya Rais Nicolas Sarkozy ya pensheni ukiingia katika siku yake ya nne. Mgomo katika kiwanda cha kusafisha mafuta ambayo hutumika katika viwanja vya ndege , umesababisha mafuta kutofika katika viwanja hivyo kupitia bomba la mafuta liendalo katika viwanja vikuu viwili vya ndege mjini Paris tangu jana Ijumaa.
Kampuni ambayo inasafirisha mafuta kupitia bomba hilo imesema kuwa uwanja mkuu wa ndege katika mji wa Paris , Charles de Gaulle, unaweza kukosa mafuta ifikapo mapema wiki ijayo. Wakati huo huo, Rais Sarkozy ametuma kikosi cha polisi wa kuzuwia ghasia ili kumaliza uzuwiaji huo wa huduma ya mafuta katika viwanda 12 vya kusafisha mafuta nchini humo. Vyama vya wafanyakazi nchini Ufaransa vinapinga mipango ya serikali ya kuongeza umri wa kustaafu.