Mfalme Mumbere wa Uganda ashitakiwa | Matukio ya Afrika | DW | 30.11.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Uganda

Mfalme Mumbere wa Uganda ashitakiwa

Mfalme wa kimila nchini Uganda Jumanne hii amefunguliwa mashitaka ya mauaji na kupelekwa kwenye kizuizi chenye ulinzi mkali, taarifa kutoka kwa afisa wa serikali zimesema.

Watu wasiopungua 149 walikamatwa kwenye makabiliano hayo yaliyotokea mwishoni mwa wiki iliyopita katika mkoa wa Rwenzori, uliopo Magharibi mwa Uganda, ambako kuna utawala wa kifalme. Majeshi ya usalama yameendelea kuwasaka watu wengine kwenye maeneo ya milimani ambako kunapatikana  waasi wengi.

Mfalme Charles Wesley Mumbere wa tawala ya kifalme ya Rwenzuru amekuwa kizuizini tangu kuvamiwa kwa ikulu yake na jeshi jumapili iliyopita. Amezuiliwa jela hadi Desemba 13, amesema msemaji wa mahakama, Solomon Muyita.

Angalau watu 46 wanaomuunga mkono mfalme huyo na polisi 16 walikufa katika makabiliano hayo, hii ikiwa ni kulingana na msemaji wa jeshi la polisi Andrew Felix Kaweesi. Kaweesi amesema pia kwamba upo uwezekano wa kuongezeka kwa idadi ya vifo wakati kutokana na makabiliano mengine yaliyotokea kwenye vijiji vingine ambayo hayakuripotiwa.

Wengi wa waliouwawa ama waliotiwa kizuizini ni walinzi waliokuwa wakimlinda Mumbere, anayetuhumiwa kwa kuwahifadhi waasi nyumbani kwake eneo la Kasese, ambalo ni ngome ya upinzani iliyoko karibu na mpaka kati ya Uganda na Kongo.

Silaha, ambazo ni pamoja na bunduki za kisasa, mishale na mapanga zimekamatwa kufuatia makabiliano hayo kwenye ikulu ya kifalme, ambayo yalifuatiwa na mapigano mengine ya siku mbili na yaliyohusisha wapiganaji wa kikabila. Waziri wa mambo ya ndani wa Uganda, Jeje Odongo amewaambia waandishi wa habari.

Uganda Rwenzori Gebiet im Westen (Getty Images/AFP/P. Martell)

Sehemu ya milima ya Rwenzori, ambapo polisi nchini Uganda inaendelea kuwasaka wapiganaji

Amnesty International yailaumu serikali ya Uganda kwa ukiukwaji wa haki za binaadamu.

Mauaji hayo yameibua wasiwasi kati ya utawala uliodumu kwa kipindi kirefu wa Rais Yoweri Museveni na viongozi wa kikabila wenye ushawishi mkubwa ambao wanatambulikana kikatiba, lakini wakikosa mamlaka kamili ama kumiliki jeshi lao. Ikiwa ni baada ya uchaguzi wa urais wa mwezi Februari na Museveni kuibuka tena mshindi, Mumbere alionekana kuungwa mkono na upinzani, hatua ambayo inavuruga maadili ya utendaji kwa viongozi wa kimila.

Museveni alipoteza umaarufu wake kwenye eneo hilo la Kasese, na mwezi mmoja baadae kulizuka mapigano kati ya vikosi vya uslama vya serikali  na wapiganaji waliomtii Mumbere. Miongoni wa wanaomuunga mkono mfalme huyo ni kikundi cha waliojitenga wanaotaraji kuunda Jamhuri mpya iitwayo Yiira, ambayo ingehusisha watu wa mfalme Mumbere wa jamii ya Bakonzo  iliyoko eneo la mpaka wa Uganda na Kongo. Kikundi hiyho kinadaiwa kutengeneza noti yake, na hata kukusanya kodi kwenye baadhi ya maeneo.

Mnamo mwezi Machi kabla ya kuibuka kwa mapigano kati ya wanaomuunga mkono Mumbere na jeshi, Museveni aliapa kuliangusha kundi hilo la waliojitenga, waliokuwa na madai kwamba serikali imewatelekeza.

Shirika la Haki za Binaadamu la Amnesty International lilisema kulikuwepo na mifano ya mauaji na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu wakati wa kuwakatamata watuhumiwa, na baadhi yao walidaiwa kuuwawa kwa kupigwa risasi na miili yao kutupwa. Kiongozi wa upinzani, Kiiza Besigye ameyataja mauaji hayo kama "mauaji ya kimbari" na kutuma picha kupitia ukurasa wake wa twitter inayoonyesha mili ya wahanga hao nje ya ikulu ya mfalme Mumbere.

Mwandishi: Lilian Mtono/AFPE
Mhariri: Daniel Gakuba

 

Matangazo

IJUE DW

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com