1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Brexit yacheleweshwa hadi Oktoba 31

Josephat Charo
11 Aprili 2019

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wamekubaliana na Uingereza siku ya Alhamisi kuchelewesha mchakato wa Brexit kwa kipindi cha hadi miezi sita.

https://p.dw.com/p/3Gbkl
Belgien Brüssel - Donald Tusk, Theresa May und Angela Merkel
Picha: picture-alliance/empics/L. Neal

Makubaliano yaliyoafikiwa katika mazungumzo yaliyoendelea hadi jana usiku mjini Brussels yana manaa, ikiwa Uingereza inabakia katika Umoja wa Ulaya baada ya tarehe 22 mwezi ujao wa Mei, wapigaji kura wa Uingereza watalazimika kushiriki katika uchaguzi wa bunge la Ulaya, ama nchi itoke katika Umoja wa Ulaya bila makubaliano yoyote.

Waziri mkuu wa Uingereza, Theresa May, amesema sasa ataendelea na jitihada zake kutaka mpango wake upitishwe na bunge kuhakikisha nchi yake inajitoa kwa njia nzuri, akisema lengo lake ni kuondoka haraka iwezekanavyo.  Bi May amesema wakati wa urefushaji wa mchakato wa Brexit, baraza la Ulaya limeweka wazi kwamba Uingereza itaendelea kuwa na haki kamili za uanachama, pamoja na majukumu yake.

"Naelewa jinsi watu wengi walivyokata tamaa kwamba nililazimika kuomba mchakato wa Brexit urefushwe. Uingereza ilitakiwa iwe imeshajitoa Umoja wa Ulaya kufikia sasa na najuta sana kwamba sijafanikiwa kulishawishi bunge kuridhia mkataba ambao ungeiwezesha Uingereza kuondoka kwa njia nzuri. Lakini sasa mambo ya kuchagua ni bayana na ratiba iko wazi. Kwa hiyo sasa lazima tuendelee kujitahidi kufikia makubaliano juu ya mkataba kwa masilahi ya taifa."

Tusk awaonya Waingereza kuhusu Brexit

Rais wa baraza la Ulaya, Donald Tusk, amewaonya Waingereza wasiitumie vibaya fursa hii mpya waliyopewa kutafuta suluhisho la mkwamo wa Brexit. "Urefushaji huu hauna masharti sana kama nilivyotarajia, na ni mfupi kidogo kuliko nilivyotarajia. Lakini hata hivyo unatosha kutafuta suluhisho bora kabisa kadri inavyowezekana. Tafadhali msipoteze fursa hii na muda huu." 

Belgien Brexit-Gipfel in Brüssel
Donald Tusk, rais wa baraza la UlayaPicha: Reuters/Y. Herman

Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, amepinga vikali urefushaji muda kwa mchakato wa Brexit, lakini viongozi wengi wameunga mkono na Wafaransa wakalazimika kukubalia ahadi kwamba ucheleweshaji huo utadurusiwa upya katika mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya unaotarajiwa kufanyika tarehe 21 mwezi Juni.

Viongozi wengi waliokusanyika katika mkutano wa dharura wa viongozi wa Umoja wa Ulaya, akiwemo kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, waliunga mkono mpango wa kuahirisha Brexit kwa muda hadi mwaka mmoja. Lakini mazungumzo yalipoendelea hadi leo asubuhi, rais Macron, akiungwa mkono na Ubelgiji, Austria na mataifa kadhaa madogo wanachama wa Umoja wa Ulaya, aliunga mkono ucheleweshaji wa Brexit kwa wiki chache tu na kutaka hakikisho thabiti kutoka wa Uignereza kwamba haitoingilia shughuli muhimu za Umoja wa Ulaya wakati wa kipindi hicho.

afpe, reuters