1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan Kusini

Mazungumzo ya amani Sudan Kusini yafanyika Nairobi

10 Mei 2024

Mazungumzo ya ngazi za juu kuhusu amani nchini Sudan Kusini yameanza jijini Nairobi nchini Kenya, huku miito ikitolewa na marais wa Afrika ya kumalizwa mzozo uliodidimiza uchumi wa taifa hilo kwa miaka kadhaa sasa.

https://p.dw.com/p/4fhFV
Rais wa sudan Kusini Salva Kiir
Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir amesema nia yao kwa sasa ni kumaliza mzozo nchini mwao na kuleta amaniPicha: Samir Bol/ZUMAPRESS/picture alliance

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir pamoja na kumshukuru mwenyeji wa mazungumzo hayo Rais William Ruto ameahidi kwamba serikali yake itafanya mazungumzo hayo kwa nia njema na kwa uwazi. Mazungumzo hayo yamefunguliwa siku ya Alhamisi.

"Makundi ya upinzani yana nia sawa na hamu ya amani nchini Sudan Kusini ambayo baada ya kupatikana kikamilifu, italeta utulivu wa wakati wote na maendeleo ya kiuchumi katika eneo hilo, na sio tu Sudan Kusini," alisema Kiir.

"Tunahitaji kuacha mawazo ya mizozo, tunatakiwa kuacha kujiona maadui. Sisi ni ndugu, Rais Kiir, sisi ni ndugu na jamaa," alisema kiongozi wa kundi la waasi la Real-SPLM Pagan Amum Okiech.

Soma pia: Mchakato wa amani Sudan Kusini hatarini: UN

Mazungumzo hayo yanayokutanisha makundi ya waasi na serikali, si sehemu ya makubaliano ya mwaka 2018 yaliyohitimisha vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka mitano na kusababisha vifo vya watu 40,000.

Soma pia: UN: Raia 440 waliuwawa katika mapigano Sudan Kusini

Ruto ayataka mataifa ya Afrika kusaka suluhu za matatizo yao yenyewe

Rais Ruto hapo jana alirudia kuzungumzia umuhimu wa kujumuisha pande zinazozozana na mara zote Afrika kusaka suluhu ya matatizo yake yenyewe.

Rais wa Malawi Lazarus Chakwera, Rais wa Zambia Hakainde Hichilema, Rais wa Namibia Nangolo Mbumba na Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Faustin Archange Touadera pia walikuwepo kwenye ufunguzi wa mazungumzo hayo uliofanyika baada ya mkutano wa kilele wa masuala ya kilimo wa Umoja wa Afrika.

Mazungumzo ya amani nchini Sudan Kusini yafanyika Nairobi
Rais wa Kenya William Ruto ameyatolea wito mataifa ya Afrika kusuluhisha matatizo yao wenyewePicha: Dominika Zarzycka/NurPhoto/picture alliance

Mwakilishi maalumu wa Marekani kwenye Pembe ya Afrika Mike Hammer aliyakaribisha mazungumzo hayo, akisema Marekani inaridhishwa na namna Kenya inavyojitolea katika masuala yanayohusu utulivu wa kikanda pamoja na kusaidia upatikanaji wa amani nchini Sudan Kusini, hii ikiwa ni kulingana na ubalozi wa Marekani nchini Kenya kupitia mtandao wa X.

Mpatanishi mkuu kwenye mazungumzo hayo Lazarus Sumbeiywo ameonyesha imani kwamba mazungumzo hayo yatafanikisha kupatikana kwa suluhu katika masuala yaliyoendelea kusababisha mivutano nchini humo. Amesema baada ya mazungumzo haya, wanapanga kuwa na mwendelezo wa majadiliano ili kuhakikisha kunapatikana suluhu pana na ya haraka ya masuala hayo, ali mradi tu pande zote zitaheshimu mpango huo.

Sudan Kusini imesalia katika hali tete licha ya makubaliano ya amani ya mwaka 2018, ambayo bado hayajatekelezwa kikamilifu hadi sasa. Taifa hilo linatarajiwa kufanya uchaguzi mwezi Disemba lakini masuala muhimu ambayo ni pamoja na kuunganisha vikosi vya usalama bado halijafikiwa makubaliano.