Mawaziri wa mazingira wawasili Warsaw kwa mazungumzo ya tabia nchi | Matukio ya Kisiasa | DW | 20.11.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mawaziri wa mazingira wawasili Warsaw kwa mazungumzo ya tabia nchi

Nchi zinazoendelea zinataka hakikisho la misaada katika majanga ya siku za usoni yatokanayo na kuongezeka kwa joto duniani huku mazungumzo ya Warsawa yakingia awamu muhimu

Mawaziri wa mazingira wa nchi mbalimbali walianza kuwasili jana mjini Warsaw wakitumai kuyapiga jeki mazungumzo hayo yanayotafuta maafikiano ya kudhibiti mabadiliko ya hewa ifikapo mwaka 2015.

Mawaziri hao hii leo watajadili masuala ya ufadhili katika duru ya kwanza ya mazungumzo ya ngazi ya juu yanayotarajiwa kudumu kwa siku mbili zijazo kuudurusu mchakato wa umoja wa Mataifa kuhusu makubaliano ya tabia nchi ujulikanao kama UNFCCC.

Nchi zinazoendelea zinazitaka nchi zilizostawi duniani kutimiza ahadi ya mwaka 2009 ya kuchangisha dola bilioni 100 kwa mwaka itakayoshughulikia masuala ya tabia nchi ifikapo mwaka 2020.

Ufadhili kwa nchi zinazoendelea wahitajika

Mpango wa mazingira wa Umoja wa Mataifa UNEP hapo jana ulisema Afrika pekee inahitaji kiasi ya dola milioni 200 kwa mwaka kuweza kukidhia mahitaji yake ya kukabiliana na mabadiliko ya hewa.

Wajumbe wa Uflipino katika mkutano wa Warsaw 2013

Wajumbe wa Uflipino katika mkutano wa Warsaw 2013

Nchi nyingi maskini duniani sadfa ndiyo pia zinakumbwa na madhara ya tabia nchi kama ukame,mafuriko,vimbunga vibaya na kupanda kwa viwango vya maji mabaharini.

Zaidi ya nchi 130 zinazoendelea sasa zinataka kuwe na mfumo wa kimataifa wa kushughulikia maafa utakaofadhiliwa na nchi tajiri.

Hata hivyo nchi hizo tajiri haziko tayari kufanya hivyo,zikihoji kuwa nchi masikini zinabeba dhamana ya kuongezeka kwa viwango vya joto kwani ndizo zilizoanza kutumia nishati ambayo inasababisha matatizo ya gesi inayochafua mazingira.

Miongoni mwa mambo mengine mfumo huo unaopendekezwa unapaswa kuzisaidia nchi zinazoendelea kuunda teknolojia na kufahamu jinsi ya kukabiliana na hatari za tabia nchi na kutoa misaada ya kifedha kuzisaidia nchi hizo kujizoa zoa tena.

Mfumo wa bima ni miongoni mwa mapendekezo yanayozingatiwa.Nchi tajiri ambazo bado zinajaribu kujikwamua kutoka mzozo wa kiuchumi zinasita kutangaza kuunga mkono mapendekezo hayo yanayotarajiwa kufikiwa mwaka 2020 na hata malengo ya muda mfupi pia yana walakini nayo.

Suala hilo nusura lisambaratishe mazungumzo ya tabia nchi mwaka jana yaliyokuwa yakifanyika Doha Qatar lakini yaliokolewa na makubaliano kuwa kutawekwa mikakati ya kitaassisi kujadiliwa kwa huu wa Warsaw.

Nchi tajiri zasita kufadhili majanga

Masuala ambayo bado yatahitaji ufafanuzi katika meza ya mazungumzo pia ni suala la iwapo nchi inayokumbwa na janga linalotokana na athari za tabia nchi je ndiyo ilaumiwe kwa kuruhusu watu kuishi katika maeneo hatari au kutotoa mikakati ya kuwalinda na kuwashughulikia baada ya majanga.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon

Kisha kuna suala la uchafuzi wa mazingira kutokana na gesi inayotoka viwandani hasa katika nchi zinazoinukia kwa kasi kama Brazil,China na India ambayo inachochea pakubwa katika ongezeko la joto duniani.

Dunia tayari inashuhudia joto la nyuzi 0.85 ambalo ni la juu sana ikilinganishwa na ilivyokuwa mwaka 1880 na wanasayansi wanaonya kuwa joto hilo litaongezeka hadi nyuzi 5.0 iwapo hatua za dharura hazitachukuliwa kupunguza kutolewa kwa gesi inayochafua mazingira.

Hapo jana katibu mku wa umoja wa Mataifa Ban Ki Moon alizihimza nchi zote kuweka mikakati madhubuti ya kupunguza gesi ya Carbon akisema ahadi ambazo zimetolewa kufanya hivyo hazitoshi kukabiliana na athari za mabadiliko ya hewa.Mkutano huo wa tabia nchi unatarajiwa kufikia ukingoni hapo kesho.

Mwandishi:Caro Robi/afp/ap

Mhariri:Oumilkheir Hamidou

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com