1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhusiano wa jinsia na mabadiliko ya tabia nchi wajadiliwa mjini Warsaw

19 Novemba 2013

Mkutano wa Kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi unaendelea mjini Warsaw, Poland, ambapo suala la jinsia na uhusiano wake katika mabadiliko hayo linajadiliwa kwa upana.

https://p.dw.com/p/1AL10
Picha: Stefan Postles/Getty Images

Jumanne (19.11.2013) ilikuwa ni siku maalum ya kuzungumzia masuala ya mabadiliko ya tabia nchi na uhusiano wake na masuala ya jinsia, ambapo wanawake wanaelezwa kuguswa moja kwa moja na mabadiliko ya tabia nchi, na hivyo kuna umuhimu wa kuwashirikisha katika ngazi ya majadiliano.

Ikiwa lengo la mkutano huo ni kujenga msingi wa kufikiwa makubaliano kuhusu suala la kupunguzwa uzalishaji wa gesi chafu kwa mataifa makubwa duniani, hata hivyo uhusiano kati ya mabadiliko ya tabia nchi na jinsia ulipewa umuhimu wakati wa mkutano huo.

Pia uzinduzi wa orodha maalum ya jinsia na mazingira chini ya usimamizi wa Shirika la Kimataifa la uhifadhi wa mazingira (IUCN), nao ulitarajiwa kufanyika.

Lorena Aguilar, mshauri wa masuala ya jinsi wa shirika hilo la uhifadhi wa mazingira ameliambia shirika la habari la IPS kuwa orodha hiyo ya aina yake itapima uwiano wa jinsia, mazingira na utawala bora, ambapo jumla ya nchi 72 zimewekwa kwenye orodha hiyo kulingana na viashiria vya mabadiliko yaliyokwishajitokeza.

Anasema orodha hiyo inapima ushiriki wa wanawake na wanaume katika mikutano ya majadiliano lakini imeangalia mambo mengine kama vile masuala ya ardhi, misitu, upatikanaji wa mikopo na umiliki wa ardhi.

Mtaalamu huyo wa masuala ya jinsia amesema orodha hiyo pia itakuwa mwongozo kwa wafadhili wa namna ya kuelekeza rasilimali zake katika maeneo ambayo yana mahitaji zaidi.

Ni vipi wanawake wahusishwe na mabadiliko ya tabia nchi?

Wakati kwa mataifa ya magharibi ni swali wanalojiuliza ikiwa kuna athari tofauti ya mabadiliko ya tabia nchi kati ya wanawake na wanaume, maeneo mengi duniani hasa yale ambayo shughuli ya kilimo hufanywa na wanawake uhusiano huo uko wazi.

Wanawake ni waathirika wakuu wa mabadiliko ya tabia nchi
Wanawake ni waathirika wakuu wa mabadiliko ya tabia nchiPicha: Getty Images

Kama inavyothibitishwa na Getrude Kenyangi kutoka shirika la kusaidia wanawake waliopo katika sekta za kilimo na mazingira nchini Uganda kuwa kutokana na magawanyiko wa majukumu, wanawake Uganda ndiyo wanaotafuta chakula, wanaolima, kukitayarisha na kuilisha familia.

Anasema chakula na maji vina uhusiano wa moja kwa moja na kama mtu atakosa vitu hivi, basi hawezi kutekeleza majukumu ya familia yake ipasavyo na hiyo itakuwa ni mwanzo wa ugomvi kati ya mume na mke na watoto watakosa chakula na hivyo kuharibu mipangilio mingi kifamilia.

Wito kwa watunga sera

Kwa upande wake, mtaalamu wa masuala ya jinsia, Anke Stock wanachotaka kuwakumbusha watunga sera ni kwamba mabadiliko ya tabia nchi yanasababishwa na shughuli za kila siku za binaadamu na yana athari kwa kila mtu, awe mwanamke au mwanaume, kinachowatofautisha ni aina ya shughuli wanazofanya.

Maeneo mengi ya dunia, wanawake wanatembea umbali mrefu kutafuta maji kutokana na miundombinu hafifu inayosababisha kupungua kwa maji.

Hivi karibuni, Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya wanawake (UN-WOMEN), lilifanya utaifiti kuhusu mfumo wa tahadhari wakati wa mafuriko Nchini Pakistan, kuangalia vipingele mbali mbali, moja ya vipengele hivyo ikiwa ni, endapo wanawake wananafasi ya kufanya maamuzi yanapotokea mafuriko kama wanaume zao hawatakuwepo.

Mikutano ya mbadiliko ya tabia nchi huwa na sura tofauti
Mikutano ya mbadiliko ya tabia nchi huwa na sura tofautiPicha: AP

Maira Zahur kutoka Pakistan anasema wanawake wengi nchini humo hawaruhusiwi kutoka nje hata kama wanaume wao watakuwa mbali, ambapo ushahidi unaonyesha kuwa wakati wa mafuriko ya mwaka 2010, wanawake hawakuruhusiwa kutoka ndani ya nyumba zao, wakati wanaume wao walipokuwa wamesafiri.

Mwandishi: Flora Nzema/IPS

Mhariri: Josephat Charo