1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wa G7 wakutana Brussels kuijadili Urusi

13 Desemba 2021

Mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya wameamua kuiwekea vikwazo kampuni ya ulinzi wa kijeshi ya Urusi-Wagner kwenye mkutano mjini Brussels leo Jumatatu.

https://p.dw.com/p/44Cpl
G7 Gipfel I Treffen der Außenminister in  Liverpool
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena BaerbockPicha: Jon Super/AP/picture alliance

Hatua hiyo imechukuliwa baada ya Umoja wa Ulaya kuionya Urusi kuwa itakabiliwa na hatua kali iwapo itaishambulia Ukraine. 

Baada ya mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi zilizoendelea kiviwanda duniani za kundi la G7 mjini Liverpool mwishoni mwa juma, ambapo waliionya Urusi kwamba itakabiliwa na hatua kali iwapo itatubuthu kuishambulia Ukraine, mawaziri hao wameamua kuiwekea vikwazo kampuni ya ulinzi wa kijeshi ya Urusi- Wagner, watu binafsi pamoja mashirika mengine yenye mafungamano na kampuni hiyo.

Miongoni mwa vikwazo hivyo ni marufuku ya kusafiri katika nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya na kufungiwa kwa mali zilizoko ndani ya Umoja huo.

Soma pia: China yaliponda kundi la G7 kwa 'upotoshaji'

Vikwazo hivyo pia inamaanisha makampuni ya Umoja wa Ulaya na hata watu binafsi hawawezi kufanya biashara na watu hao waliowekewa vikwazo au kampuni hiyo ya ulinzi wa kijeshi ya Urusi, Wagner.

Vikwazo hivyo aidha vinaanza kutumika kuanzia leo Jumatatu baada ya kuchapishwa katika gazeti rasmi la Umoja wa Ulaya.

Ijumaa iliyopita, afisa mwandamizi wa Umoja wa Ulaya aliliambia shirika la habari la dpa kuwa vikwazo hivyo viliwekwa kutokana na shughuli za kampuni ya Wagner nchini Syria, Libya, Ukraine pamoja na uwepo wa madai ya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.

Soma zaidi: Marais Xi wa China, Putin wa Urusi waibua changamoto kwa G7

Kulikuwa na wasiwasi pia ndani ya Umoja wa Ulaya juu ya uwezekano wa Wagner kutumwa nchini Mali. Wanachama wa Umoja wa Ulaya wametishia kusitisha msaada wao kwa serikali ya Mali iliyokumbwa na mzozo, iwapo kampuni ya Wagner ingepewa kandarasi kufanya oparesheni zake nchini humo.

Ama kuhusu kususia kidiplomasia michezo ya Olimpiki ya msimu wa baridi kutokana na wasiwasi juu ya rekodi ya haki za binadamu nchini China, baadhi ya mataifa ya Ulaya yameonyesha kusita sita kuiunga mkono Marekani katika kususia michezo hiyo.

Waziri wa mambo ya nje wa Austria Alexander Schallenberg amesema, "Kuingiza silaha kwenye michezo sioni kama kuna umuhimu wowote" mwisho wa kumunukuu.

Naye Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock ameliambia shirika la habari la Ujerumani la ZDF kuwa wanariadha hujitayarisha kwa miaka kwa ajili ya michezo ya Olimpiki na kwa hivyo michezo ya Olimpiki haipaswi kuingizwa siasa.

Mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya walikuwa wanatafuta msimamo wa pamoja juu ya suala hilo baada ya wiki iliyopita Ufaransa kusema kususia kwa viongozi na mabalozi wa Umoja huo katika hafla ya ufunguzi wa michezo ya Olimpiki kutakuwa na athari ndogo.