Mauaji Kusin mwa Sudan | Matukio ya Kisiasa | DW | 22.09.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mauaji Kusin mwa Sudan

Watu mia moja wauwawa Kusini mwa Sudan

default

Mwanajeshi wa Kijerumani wa kulinda amani Kusini mwa Sudan akiwa mjini Juba

Zaidi ya watu 100 wameuawa katika mapigano ya mwishoni mwa wiki kwenye jimbo lenye vurugu la Jonglei lililopo kusini mwa Sudan, ambapo kiwango cha vifo vinavyosababishwa na vurugu hizo kimepindukia kile cha Darfur.

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Ukombozi la Watu wa Sudan (SPLA) Kuol Diem Kuol, ameliambia Shirika la Habari la AFP kuwa, kuna jumla ya watu 102 waliouawa, wakiwemo raia 53, washambuliaji 23 na 46 kujeruhiwa.

Awali kamanda huyo aliiambia AFP kuwa, wakati idadi ya vifo ilipokuwa 76, 11 kati ya waliokufa ni askari wa SPLA, na 11 wengine walikuwa ni askari wa vikosi vingine.

Alisema kuwa haukuwa uvamizi dhidi ya ng'ombe, bali ni shambulizi la wanamgambo dhidi ya vikosi vya usalama.

Watu wa kabila la Lou Nuer walivamia kijiji cha Dinka Hol cha Duk Patiet katika jimbo la Jonglei jumapili asubuhi, na kulazimisha kundi la askari wa SPLA walioko katika eneo hilo kukimbia.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, zaidi ya watu 2000 wameuawa na wengine 250,000 kupoteza makazi yao katika mapigano ya makazi katika eneo la kusini la nchi hiyo, tangu mwezi Januari, huku vifo vinavyotokana na machafuko hayo vikipindukia idadi ya vifo katika eneo lililoharibiwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe la Darfur, lililopo magharibi mwa Sudan.

Duru moja nchini humo imesema kuwa mkutano wa maridhiano kati ya makabila makubwa katika jimbo la Jonglei ulipangwa kufanyika tarehe 30 mwezi wa Septemba, lakini umeahirishwa.

Mapigano baina ya vikundi vya makabila katika eneo la kusini mwa Sudan huripuka mara kwa mara, mara nyingi yakichochewa na wizi wa ng'ombe na mabishano juu ya mgawanyo wa rasilimali asilia, wakati wengine wapo katika harakati za kulipiza kisasi kutokana na mashambulizi ya awali.

Hata hivyo mlolongo wa hujuma za hivi karibuni umewashtua wengi, huku mashambulizi dhidi ya wanawake na watoto yakionekana kuongezeka.

Awali kamanda Kuol alisema kuwa anadhani uvamizi wa jumapili, ulisaidiwa na wafuasi wa chama kinachotawala Kaskazini mwa Sudan cha National Congress Party (NCP).

Maafisa wa NCP mara kadhaa wamepinga tuhuma hizo.

Hali ya wasiwasi Kaskazini mwa Sudan bado iko juu, huku Sudan ikiwa imegawanywa na udini, ukabila na tofauti za kiitikadi, vyote vikiwa vimechochea vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka 22, hadi mwaka 2005 mpango wa amani uliposainiwa.

Katika mpango huo wa amani, upande wa kusini wa nchi hiyo una kipindi cha mpito cha miaka sita cha kujitawala, na inashiriki katika serikali ya muungano hadi mwaka 2011.

Sudan Kusini na Kaskazini, zimekubaliana katika maeneo 10 muhimu ya kufanya kazi pamoja, ikiwa ni pamoja na uchaguzi mkuu wa mwezi April, juhudi za amani katika jimbo la Darfur, kuweka mpaka wa kusini na kaskazini pamoja, na utawala wa mseto.

Mwandishi: Lazaro Matalange/AFP

Mhariri:M.Abdul-Rahman

 • Tarehe 22.09.2009
 • Mwandishi Lazaro Matalange
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Jmb2
 • Tarehe 22.09.2009
 • Mwandishi Lazaro Matalange
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Jmb2

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com