1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matokeo ya uchaguzi wa rais Congo Kinshasa yatarajiwa

Oumilkheir Hamidou
9 Januari 2019

Matokeo ya awali ya uchaguzi wa rais katika jamhuri ya kidemokrasi ya Congo yanatarajiwa kutangazwa wakati wowotwe. Mgombea wa upinzani Martin Fayulu ametahadharisha dhidi ya kutangazwa matokeo ambayo si ya kweli.

https://p.dw.com/p/3BEOo
DRCONGO-POLITICS-KABILA
Picha: Getty Images/AFP/J. D. Kannah

"Ni kazi kubwa ambayo haiwezi kukamilika kwa muda wa masaa machache tu" amesema mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi-CENI, Corneille Nangaa na kuashiria uwezekano wa matokeo ya awali  kutangazwa masaa 24 hadi 48 yanayokuja.

Kikao cha hadhara cha Ceni kimeanza tangu jana  usiku kuchunguza kwa uangalifu na kupanga kuchapisha matokeo ya awali wakati wowote kutoka sasa.

Kiongozi  wa muungano wa upande wa upinzani-Lamuka, Martin Fayulu ameonya dhidi ya kuchapishwa matokeo ambayo si ya kweli na kusema:"Ikiwa matokeo hayatalingana na ukweli wa mambo, basi tutachapisha yale tulio nayo na ambayo tayari yanajulikana na tume huru ya uchaguzi, na wasimamizi wa kimataifa, wasimamizi wa Umoja wa Africa, wasimamizi wa humu nchini, makanisa ya kikatoliki na kiprotestanti na zaidi kuliko wote, wananchi wa Congo. Na hasa wakongomani. Wananchi hawatokubali matokeo ya udanganyifu."

Wakongomani wanasherehekea hata kabla ya matokeo kutangazwa
Wakongomani wanasherehekea hata kabla ya matokeo kutangazwaPicha: Reuters/O. Acland

Onyo dhidi ya matokeo ya uwongo latolewa pia na Félix Tshisekedi

Ripota wa shirika la habari la Ufaransa AFP anasema njia inayoelekea  makao makuu ya Ceni-Boulevard du 30 juin iifungwa jana usiku na polisi waliobeba silaha baada ya Ceni kutangaza uwezekano wa kutangaza matokeo ya awali ya uchaguzi wa rais wakati wowote kutoka sasa.

Wagombea watatu wakuu wanasubiri kujua nani kati yao ameibuka na ushindi;mteule wa chama tawala, waziri wa zamani wa mambo ya ndani Emmanuel Ramazani Shadary, na viongozi wawili wa upande wa upinzani Martin Fayulu na Félix Tshisekedi.

Chama cha upinzani cha UDPS cha Félix Tshisekedi nacho pia kimeitahadharisha tume huru ya uchaguzi dhidi ya njama yoyote ya kubadilisha uamuzi wa wananchi. Njia ya ukweli inapitia katika vituo 179 kunakokusanywa matokeo-CLCR kabla ya kuwasilishwa katika tume ya Ceni.

Katibu mkuu wa taasisi hiyo Jean-Marc Kabund hakukanusha "uvumi eti rais anaemaliza wadhifa wake amefikia makubaliano pamoja na mgombea wa chama cha UDPS-Félix Tshisekedi. Amesema tu Félix Tshisekedi anapewa nafasi nzuri ya kushinda uchaguzi wa rais na kwamba Tshisekedi na Kabila wana wajib wa kukutana ili kuandaa utaratibu wa amani na wa kistaarabu wa kukabidhi madaraka."

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP

Mhariri :Yusuf Saumu