Mataifa yamkosoa Assad na hotuba yake | Matukio ya Kisiasa | DW | 07.01.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mataifa yamkosoa Assad na hotuba yake

Taasisi na mataifa mbalimbali duniani yamepinga hotuba ya Rais Bashar al-Assad wa Syria aliyoitoa Jumapili (6.1.2013) na kusema ni lazima angátuke ili kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoendelea nchini mwake.

Syria's President Bashar al-Assad speaks at the Opera House in Damascus in this still image taken from video January 6, 2013. REUTERS/Syrian TV via Reuters TV (SYRIA - Tags: POLITICS PROFILE TPX IMAGES OF THE DAY) NO SALES. NO ARCHIVES. FOR EDITORIAL USE ONLY. NOT FOR SALE FOR MARKETING OR ADVERTISING CAMPAIGNS. THIS IMAGE HAS BEEN SUPPLIED BY A THIRD PARTY. IT IS DISTRIBUTED, EXACTLY AS RECEIVED BY REUTERS, AS A SERVICE TO CLIENTS. SYRIA OUT. NO COMMERCIAL OR EDITORIAL SALES IN SYRIA

Bashar al-Assad Rede TV Fernsehen Staats TV

Katika hotuba hiyo Rais al-Assad amefuta uwezekano wa kuwa na mazungumzo na makundi ya upinzani ambayo ameyaita kuwa ni "vibaraka" wa mataifa ya magharibi na ameapa kuendelea kupambana na "magaidi" na "magenge ya wahuni " wanaotaka kuangusha utawala wake.

Akizungumza katika hotuba yake ya kwanza kwa umma baada ya kipindi cha zaidi ya miezi saba, Rais Assad amewaita wapinzani wake kuwa ni maadui wa wananchi na maadui wa Mungu ambao wameamua kufanya ugaidi.

Tunapambana na magaidi: Assad

Viongozi wa Muungano wa Upinzani wa Syria

Viongozi wa Muungano wa Upinzani wa Syria

Assad ameongeza kusema kwamba wapinzani wanaziita harakati zao kuwa ni mapinduzi lakini kumbe wanachokifanya hakihusiani kabisa na mapinduzi.

"Haya sio mageuzi kwasababu mageuzi kwa kawaida ni harakati za watu na sio vita vya wageni dhidi ya watu. Mapinduzi ni kusimama kwa ajili ya watu na sio dhidi ya watu. Hawa si wanamapinduzi, hawa ni baadhi tu ya wahalifu wa kawaida", alisema Assad.

Wafuasi wake waliokuwa kwenye ukumbi wa jengo la michezo ya kuigiza mjini Damascus walimkatiza mara kwa mara kwa kumshangilia kwa mayowe huku wakisema "Kwa roho na damu yetu tutakulinda Assad."

Katika hotuba hiyo Rais Assad alitaja mpango wa kumaliza vita vinavyoendelea nchini mwake ambao unajumuisha kufanyika kwa mjadala wa kitaifa wa mazungumzo ya amani, chaguzi za bunge na kuandikwa katiba mpya.

Pingamizi dhidi ya Asad

Mara baada ya hotuba ya kiongozi huyo, makundi ya upinzani nchini Syria yalipaza sauti na kukataa mapendekezo yake na kusisitiza kwamba ufumbuzi wa kisiasa kwa mzozo huo hauwezi kufikiwa bila ya kujiuzulu kwa kiongozi huyo. Rami Abdel Rahman mkuu wa Shirika la Kuangalia Hali za Haki za Binaadamu nchini Syria amesema hakuna nafasi ya kufikia suluhisho wakati serikali hiyo ikiwa madarakani.

Mbali na pingamizi kutoka kwa wapinzani, taasisi za kimataifa na mataifa mbalimbali nayo yamempinga Assad ukiwemo Umoja wa Ulaya. Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja huo Catherine Ashton amesema kuwa Rais Assad ni lazima aachie madaraka ili kurejesha hali ya utulivu na amani nchini Syria.

Catherine Ashton, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya

Catherine Ashton, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya

Ashton amesema kuwa wataichambua kwa makini hotuba ya Assad kuona kama kuna kitu kipya lakini msimamo wao unabaki palepale kwamba inabidi ang´atuke na kuruhusu mchakato wa kuanzisha kipindi cha kisiasa cha mpit

Kama ilivyo kwa Ashton, naye Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron alikuwa na haya ya kusema

Naye Waziri wa mambo ya Nje wa Ujerumani Guido Westerwelle ametoa wito kwa Rais Assad kuviamuru vikosi vyake vya usalama kusitisha mauwaji badala ya kuendelea kutoa hotuba hewa juu ya utayari wake wa kusitisha mapigano. Westerwelle amziita kauli za Assad katika hotuba yake kuwa ni "tupu".

Westerwelle anasema kuwa mwezi Novemba mwaka jana Rais Assad alikiambia kituo cha televisheni cha Urusi kuwa hataondoka nchini humo kwenda uhamishoni kama ilivyosemekana na kwamba ataishi na kufa ndani ya Syria.

"Ujumbe wangu kwa Assad ni “ondoka”. Ana damu nyingi za watu mikononi mwake. Sasa tunajua kuwa watu 60,000 wameuawa Syria. Nimekutana na badhi ya wakimbizi kambini kwenye mpaka wa Jordan. Mambo waliyonieleza yalinishtua sana kuhusu jinsi gain walivyopigwa kwa mabomu na risasi na wakati mwingine hata kutolewa nje ya nyumba zao, vijiji vyao na miji yao"

David Cameron, Waziri Mkuu wa Uingereza

David Cameron, Waziri Mkuu wa Uingereza

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza William Hague ameandika kwenye mtandao wa Twitter kwamba hotuba ya Rais Assad "imepindukia unafiki " na ahadi zake tupu hazitamghilibu mtu yeyote.

Hotuba hiyo imekosolewa pia na Marekani, na Uturuki ambapo zimetoa wito kwa Umoja wa Mataifa kuingilia kati na kumtoa Assad madarakani. Licha ya hayo yote, hii leo vikosi vya serikali ya Assad vimefanya mashambulizi mapya katika vitongoji mbalimbali vya mji mkuu Damascus.

Mwandishi: Mohamed Dahman/Stumai George/Dpa/Afp
Mhariri: Yusuf Saumu

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com