1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel: Wanamgambo 140 wauawa katika hospitali ya al-Shifa

21 Machi 2024

Mashambulizi ya Israel huko Gaza yamejikita katika hospitali kubwa zaidi katika ukanda huo ya al-Shifa ambapo mamia ya watu wameuawa, huku juhudi za kufikiwa makubaliano ya usitishwaji mapigano zikiendelea.

https://p.dw.com/p/4dxmS
Ukanda wa Gaza | Wapalestina wakiomboleza katika hospitali ya Al-Shifa
Wapalestina wakiomboleza vifo vya ndugu na jamaa zao kwenye makaburi katika Hospitali ya Al-Shifa katika Ukanda wa Gaza, Desemba 31, 2023. Ofisi Kuu ya Takwimu ya Palestina inasema Wapalestina wengi zaidi waliuawa katika migogoro huu ulioanza Oktoba 7, 2023 kuliko mwaka mwingine wowote tangu 1948.Picha: Mohammed Ali/Xinhua/picture alliance

Maafisa wa Israel wamesema hii leo kuwa zaidi ya wanamgambo 140 wameuawa katika siku nne za mapigano ndani na karibu ya hospitali hiyo ya al-Shifa, huku operesheni ya jeshi la Israel ikiwa bado inaendelea eneo hilo.

Waziri Mkuu wa Israel  Benjamin Netanyahu  ameapa kuliangamiza kabisa kundi la Hamas ambalo linazingatiwa kuwa la kigaidi na Umoja wa Ulaya, Ujerumani na mataifa kadhaa ya Magharibi.

Netanyahu amekuwa pia akikaidi miito ya Jumuiya ya Kimataifa iliyomtaka kuachana na mpango wake wa kuishambulia Rafah lakini amesema maandalizi ya operesheni ya kijeshi katika eneo hilo la kusini mwa Ukanda Gaza, huenda ikachukua muda kidogo.

Soma pia:Watu 90 wafariki katika operesheni ya Israel Al Shifa 

Licha ya kuwa mshirika mkuu wa Israel, Marekani imetangaza mara kadhaa kupinga  mpango huo wa kulishambulia eneo la Rafah ambalo limekuwa kimbilio la Wapalestina zaidi ya milioni 1.2 walioyahama makazi yao kufuatia mapigano ambayo tayari yamesababisha vifo vya watu 31,988; hii ikiwa ni kulingana na wizara ya afya inayodhibitiwa na Hamas.

Juhudi za kufikiwa makubaliano ya usitishwaji mapigano

Saudi Arabia- Jeddah | Antony Blinken akiwa na Mohammed bin Salman
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken akiwa kwenye mazungumzo na Mrithi wa Ufalme wa Saudia, Mohamed bin Salman mjini Jeddah: 20.03.2024Picha: Evelyn Hockstein/AFP/Getty Images

Washington imekuwa pia mstari wa mbele katika kupiga jeki juhudi za kufikiwa makubaliano ya usitishwaji mapigano. Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken ameanza hapo jana ziara yake ya sita katika eneo la Mashariki ya Kati tangu kuanza kwa mzozo huu Oktoba 7.

Jana alikuwa nchini Saudi Arabia na alikutana  na Mrithi wa Ufalme wa Saudia, Mohamed bin Salman na waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo Mwanamfalme Faisal bin Farhan kujadili mzozo wa kiutu wa Gaza na juhudi za kuongeza msaada kwa Wapalestinana, baadaye anatarajia kuelekea huko Israel baada ya ziara fupi nchini Misri.

Soma pia: UN: Hali katika hospitali za Gaza ni mbaya mno

Akiwa mjini Brussels nchini Ubelgiji kwa mazungumzo na viongozi wa Ulaya hapo jana, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema:

" Vita vinaendelea huko Gaza. Hakuna kinachoweza kuhalalisha vitendo vya kuchukiza vya Hamas mnamo Oktoba 7, na hakuna kinachoweza pia kuhalalisha adhabu ya pamoja ya watu wa Palestina. Leo, zaidi ya nusu ya idadi ya mamilioni ya watu wanakabiliwa na njaa, kulingana na ripoti iliochapishwa hivi karibuni. Na kwa hivyo lazima tuchukue hatua sasa kabla hatujachelewa..."

Aidha, Waziri Blinken amesema Marekani imewasilisha kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa rasimu ya azimio inayopendekeza kusitishwa mara moja kwa mapigano sambamba na kuachiliwa kwa mateka wa Israel wanaoshikiliwa na kundi la Hamas, na amesema ana matumaini kuwa nchi nyingi zaidi zitaunga mkono azimio hilo.

(Vyanzo: Mashirika)