1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Qatar: Makubaliano ya Gaza kuanza siku ya Ijumaa

Lilian Mtono
23 Novemba 2023

Serikali ya Qatar imesema makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Hamas yataanza kutekelezwa kesho Ijumaa. Makubaliano hayo yataanza kutekelezwa majira ya saa moja za asubuhi.

https://p.dw.com/p/4ZN8c
Gaza - Jeshi la Israel lafanya mashambulizi ya ardhini dhidi ya Hamas kaskazini mwa Gaza
Vifaru vya Israel vikirandaranda katika Jiji la Gaza, wakati wa operesheni ya ardhini inayoendelea ya jeshi la Israel dhidi ya kundi la Hamas, katika Ukanda wa Gaza, Novemba 22, 2023.Picha: Ronen Zvulun/Reuters

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Qatar ambaye ni mpatanishi mkuu kwenye makubaliano hayo, Majed al-Ansari amesema kundi la kwanza la mateka 13 litaachiliwa majira ya saa kumi za Alfajiri na kuongeza kuwa tayari wamepokea orodha ya raia wanaotakiwa kuachiliwa.

Baraza la Kivita la Israel liliidhinisha siku ya Jumatano usitishwaji wa siku nne wa mapigano, ili badala yake mateka 50 wanaoshikiliwa Gaza waachiliwe.

Qatar inatangaza haya wakati familia za mateka hao nchini Israel wakiwa na shauku kubwa ya kusikia muda huo unatangazwa ili hatimaye kukutana na wapendwa wao. 

Soma pia:Marekani na Qatar kufanikisha mpango wa makubaliano Gaza?

Nchini Israel kwenyewe, Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu amemwambia Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza David Cameron hii leo kwamba atahakikisha analiangamiza kundi la Hamas, walipozungumza katika mkutano na waziri huyo, aliyekwenda Jerusalem baada ya kutangazwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Hamas.

Cameron alisema, "Mateka wote ni lazima waachiliwe na ninatumaini kila anayehusika kwenye makubaliano haya anaweza kufanya hivyo ili kuleta ahueni kwa familia zao. Na kwa hivyo hebu tuamini kwamba hilo linaweza kufanikiwa."

Ukanda wa Gaza | Watoto wachanga walihamishwa
Muuguzi akiwahudumia watoto wachanga wa Kipalestina waliozaliwa kabla ya wakati walioletwa kutoka Hospitali ya al Shifa katika Jiji la Gaza, Ukanda wa Gaza, 19.11.2023.Picha: Hatem Ali/AP Photo/picture alliance

soma pia: Baraza la mawaziri la Israel laidhinisha makubaliano ya kuachiliwa kwa mateka

Vikosi vya IDF vyamkamata mkurugenzi wa Hospitali ya al-Shifa

Katika hatua nyingine, vikosi vya Israel, IDF mchana huu vimemkamata mkurugenzi wa hospitali ya al-Shifa Dr. Mohammed Abu Selmia huko Gaza. IDF imedai kwenye mitandao ya kijamii kwamba hospitali hiyo imekuwa ikitumiwa na Hamas kama kamandi ya kijeshi chini ya uongozi wa mkurugenzi huyo, aliyekamatwa kwa ajili ya mahojiano.

Taarifa ya IDF imesema chini ya uongozi wa Selmia, kundi hilo la Hamas limekuwa likiendesha shughuli zake za kigaidi. Muda mfupi kabla ya taarifa hiyo, msemaji wa IDF Peter Lerner ameiambia DW kwamba Abu Selmia anatakiwa kuhojiwa ili kutoa majibu ya kile anachokijua na asichokijua.

Hamas limelaani vikali kukamatwa kwa mkurugenzi huyo wa al-Shifa na idadi kubwa ya watumishi waliobakia kwenye hospitali hiyo kuendelea kuratibu utaratibu wa kuwaondoa wagonjwa ambao bado wapo pamoja na majeruhi. Mkuu wa idara moja kwenye hospitali hiyo Khalid Abu Samra pia ameliambia shirika la habari la AFP kwamba baadhi ya madaktari waandamizi wamekamatwa.

Tukiyageukia sasa mashambulizi, vikosi vya IDF vimesema wanajeshi wake wameshambulia zaidi ya maeneo 300 ya Hamas katika Ukanda wa Gaza katika kipindi cha siku moja. Maeneo hayo ni pamoja na kamandi za kijeshi, mahandaki ya chini ya ardhi na maghala ya kuhifadhia silaha.