Marekani yatakiwa kuheshimu makubaliano ya nyukilia
13 Oktoba 2017Sigmar Gabriel ameonya kuwa iwapo Marekani itajiondoa au kuchukua hatua yoyote kinyume cha makubaliano hayo basi hatua hiyo italeta athari kati ya Marekani na nchi za ulaya na kutoa mwito kwa mataifa ya ulaya kuwa na msimamo wa pamoja katika suala hilo pamoja na kuchukua hatua muhimu na za haraka.
Rais Trump anatarajia kutangaza hii leo mikakati mipya kufuatilia uwezo wa Iran kuhusiana na nguvu za nyukilia ambapo anatarajiwa pia kutangaza kuwa Marekani haina masilahi na makubaliano hayo ya kihistoria yaliyofikiwa mwaka 2015.
Hata hivyo maafisa wa Marekani wanasema Trump hatatangaza rasmi kutoyatambua makubaliano hayo bali ataelezea jinsi asivyokubaliana na jinsi Iran inavyoyatekekeleza na kuliachia bunge kuamua.
Makubaliano hayo yalisainiwa mwaka 2015 kati ya Iran na nchi sita zenye nguvu duniani ambazo ni pamoja na Marekani, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na Urusi.
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Sigmar Gabriel amewaeleza wachapishaji magazeti wa kampuni ya RND kuwa wanapaswa kuwaeleza wamarekani kuwa mwenendo wao kuhusiana na suala hilo utasababisha mataifa ya ulaya kuwa na msimamo wa pamoja na Urusi na China dhidi ya Marekani.
Trump mara kadhaa amekuwa akitahadharishwa na viongozi wa kidunia na pia ndani ya uatawala wake juu ya umuhimu wa kuheshimu makubaliano hayo ya nyukilia.
Iran iliondolewa vikwazo vya kiuchumi
Makubaliano hayo yalishuhudia Iran ikiondolewa vikwazo vya kiuchumi vilivyokuwa vimewekwa dhidi yake ambapo Iran nayo kwa mujibu wa makubaliano hayo ilipaswa kuacha kuendeleza mipango yake ya kuwa na silaha za nyukilia.
Hata hivyo shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya nyukilia mara kadhaa limekuwa likisisitiza kuwa Iran imekuwa ikitekeleza makubaliano hayo licha ya rais Trump kudai kuwa Iran inakiuka makubaliano ya nyukilia kutokana na kumuunga moono rais wa Syria Bashar al-Assad pamoja na kufanya jaribio la kurusha kombora la masafa.
Marekani inaitaka Iran kuhakikisha kuwa inaacha kuchochea migogoro nchini Syria, Iraq au Yemen lakini Gabriel anasema hilo halipaswi kuwa sharti la kuibana Iran isijihusishe na mpango wa kuwa na silaha za nyukilia.
Rais wa Iran Hassan Rouhani amemshutumu Trump kuwa anapingana na dunia kutokana na kujaribu kujitenaga na makubaliano hayo ya kihistoria. Rouhani ameongeza kuwa sasa itafahamika wazi kuwa ni nchi gani inafuata sheria na nchi gani inaheshimika kimataifa.
Hadi Jumapili Trump alikuwa hajaliarifu bunge la nchi hiyo iwapo anaamini kuwa Iran inatekeleza makubaliano ya nyukilia yaiyofikiwa kati yake na nchi sita zenye nguvu duniani.
Iwapo Trump atakataa kukubali kuwa Iran inatekeleza makubaliano hayo basi bunge litapaswa kuamua katika muda wa siku 60 ni vikwazo gani vipya viwekwe dhidi ya Iran.
Mwandishi: Isaac Gamba/dw/afpe
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahaman