1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani imeshindwa kuidhibiti Iran-Ali Khamenei

Daniel Gakuba
3 Novemba 2018

Kiongozi mwenye mamlaka ya juu nchini Iran Ayatollah Ali Khamenei amesema Marekani imeshindwa kuidhibiti Iran tangu yalipotokea mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1979, ambayo yaliiondoa serikali iliyoungwa mkono na Marekani.

https://p.dw.com/p/37bkE
Ali Khamenei, Irans Religionsführer in Azadi-Stadion
Picha: khamenei.ir

 

Katika mkutano  na kundi la wanafunzi mapema Jumamosi, Ali Khamenei amesema sera za Rais Donald Trump wa Marekani zinakabiliwa na upinzani mkubwa duniani kote, wakati Washington ikijiandaa kurejesha vikwazo kwa biashara ya mafuta ya Iran, na kwa sekta ya fedha ya nchi hiyo.

''Dunia inapinga kila uamuzi unaofanywa na Trump,'' amesema Khamenei akinukuliwa na kituo cha televisheni ya taifa ya Iran wakati wa mazungumzo yake na maelfu ya wanafunzi. Kiongozi huyo wa kiroho ameongeza kwamba Marekani imeshindwa na Jamhuri hiyo ya Kiislamu, katika juhudi zake za kuiyumbisha Iran katika kipindi cha miaka 40 iliyopita.

Marekani kuibana tena Iran kwa vikwazo

Jumatatu wiki ijayo, Marekani itaanza kutekeleza vikwazo vikali dhidi ya Iran, kwa nia ya kuilazimisha nchi hiyo kuingia katika mazungumzo ya kuachana na mpango wake wa nishati ya atomiki na mradi wa makombora ya masafa marefu, na kuacha kuyaunga mkono makundi ya wapiganaji katika mizozo ya Mashariki ya Kati.

USA Washington Donald Trump zum Fall Khashoggi
Rais wa Marekani Donald Trump ana msimamo mkali dhidi ya IranPicha: picture-alliance/dpa/AP/E. Vucci

Hata hivyo, utawala wa Trump ulisema Ijumaa kwamba nchi 8 zitaruhusiwa kuendelea kununua mafuta ya Iran hata baada ya tarehe ya kuanza upya kwa vikwazo hivyo.

Uturuki imesema imepata dalili kutoka kwa Marekani kwamba ni miongoni mwa nchi 8 zitakazofumbiwa macho, ikisisitiza hata hivyo kwamba inasubiri kupata maelezo yanayoeleweka zaidi.

Sehemu kubwa ya vikwazo dhidi ya Iran ilikuwa imeondolewa mwanzoni mwa 2016 baada ya makubaliano kuhusu mpango wake wa nyuklia yaliyofikiwa baina ya nchi hiyo na mataifa yenye nguvu duniani mwaka, lakini Trump aliiondoa nchi yake katika makubaliano hayo.

Ulaya yajaribu kusimama na Iran

Balal offshore Bohrinsel im Persischen Golf
Sekta muhimu ya mafuta ya Iran ndio shabaha kuu ya vikwazo vya MarekaniPicha: Getty Images/B. Mehri

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Iran Mohammed Javad Zarif amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini, na mawaziri wenzake wa Ujerumani, Sweden na Denmark, kuhusu hatua za Umoja wa Ulaya za kupinga vikwazo hivyo vipya vya Marekani.

Shirika la habari la Iran, IRNA, limesema Bi Mogherini na mawaziri hao wa nchi za Ulaya, wameendelea kuzingatia majukumu ya kifedha ya umoja huo katika kuyanusuru makubaliano kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.

Duru za kidiploasia zimeliambia shirika la habari la Reuters kwamba hatua za Umoja wa Ulaya za kurahisisha malipo ya kifedha kwa mafuta ya Iran zitaanza kuwa na nguvu kisheria kuanzia Jumapili tarehe 4 Novemba 2018, lakizi hazitaanza kutekelezwa rasmi hadi mwanzoni mwa mwaka ujao.

Mwandishi: Daniel Gakuba/rtre, ape

Mhariri: Jacob Safari