Mapinduzi ya Mali yalaaniwa ndani na nje ya bara la Afrika | Matukio ya Afrika | DW | 19.08.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Mali

Mapinduzi ya Mali yalaaniwa ndani na nje ya bara la Afrika

Watu nchini Mali wanajaribu kurejea katika hali ya kawaida baada ya rais Ibrahim Boubacar Keita kujiuzulu kutokana na wanajeshi walioasi kuiangusha serikali yake.Hatua ya wanajeshi hao imelaaniwa ndani na nje ya Afrika.

Msemaji wa wanajeshi hao waasi ameeleza kuwa wamechukua hatua hiyo ili kuiepusha Mali kutumbukia katika vurumai kubwa zaidi. Amesema sababu ya kuipindua serikali ni kurejesha utulivu na kusimamia kipindi cha mpito cha kuelekea kwenye uchaguzi katika muda utakaofaa. Hata hivyo hatua ya wanajeshi hao waasi imelaaniwa mara moja na viongozi wa kanda yote ya Sahel, Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya na Umoja wa Mataifa.

Waziri wa mambo ya nje wa Niger iliyomo kwenye jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS Kalla Ankourao amesikitishwa na hatua iliyochukuliwa na wanajeshi wa Mali ya kumwangusha rais Keita.Waziri huo ameiambia DW kwamba kwa muda wa miezi miwili wamekuwa wanajaribu kusuluhisha na walitumai kwamba watu wa Mali wangezifuata kanuni za jumuiya ya ECOWAS ambazo ni za demokrasia na utawala bora lakini kuangushwa serikali kumeyakomesha mazungumzo hayo kwa njia ya kikatili.

Rais wa Mali aliyelazimishwa kujiuzu Ibrahim Boubacar Keita

Rais wa Mali aliyelazimishwa kujiuzu Ibrahim Boubacar Keita

Waziri huyo wa Niger ambayo kwa sasa ni mwenyekiti wa Ecowas amesema wanajeshi wa Mali wamechukua hatua hiyo wakati mbaya. Ameeleza kuwa nchi za ECOWAS zilihitaji muda ili kuweza kuyashughulikia matatizo ya kina kirefu katika uongozi wa nchini Mali. Amesema nchi hizo zilikuwa zinakaribia kupata suluhisho.

Mwezi uliopita Jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi iIlipendekeza kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa na kuahidi kuendelea kumsaidia rais Keita, lakini pendekezo hilo lilitupiliwa mbali na wapinzani.

Jumuiya ya ECOWAS yenye nchi wanachama 15 imesema itafunga mipaka yake ya ardhini na ya angani kwa Mali na imesema itasisitiza kuwekwa vikwazo dhidi ya wanajeshi walioipindua serikali. Mali pia itasimamishwa kushiriki kwenye taasisi za maamuzi za jumuiya hiyo ya kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litaitisha kikao cha dharura kuujadili mgogoro wa Mali. Ufaransa na Niger zimeomba kuitishwa kikao hicho. Mwanadiplomasi mmoja mwandamizi wa Umoja wa Mataifa ameliambia shirika la habari la AP kwamba kikao hicho kitakuwa cha faragha.

Vyanzo:/AFP/RTRE