1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano yazuka Kivu Kusini baada ya makubaliano ya amani

17 Novemba 2025

Siku chache baada ya kusainiwa makubaliano ya amani kati ya Kinshasa na waasi wa AFC/M23 mjini Doha, mapambano makali yanashuhudiwa katika baadhi ya vijiji ndaji ya jimbo la Kivu Kusini kati ya Wazalendo na AFC/M23.

https://p.dw.com/p/53kxT
Qatar Doha 2025 | Wawakilishi wakipeana mikono baada ya kusaini makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Kongo na M23
Mpatanishi wa amani Sumbu Sita Mambu kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (Kushoto), na katibu mtendaji wa kundi la M23 linaloungwa mkono na Rwanda Benjamin Mbonimpa (Kulia) wakipeana mikono baada ya kusaini makubaliano ya kusitisha mapigano katika mji mkuu wa Qatar, Doha mnamo Julai 19, 2025Picha: Mahmud Hams/AFP

Mapambano hayo yameshuhudiwa tangu Jumatatu asubui katika baadhi ya vijiji karibu na mbuga ya wanyama ya Kahuzi-Biega, ndaji ya jimbo la Kivu Kusini kati ya Wazalendo na AFC/M23. Mapambano mengine yameripotiwa Kivu kaskazini siku ya Jumapili, hali inayowapa wakazi maswali mengi kuhusu makubaliano hayo.

Mashuhuda katika baadhi ya vijiji hivyo wanaeleza kwa masikitiko kwamba milio ya silaha nzito-nzito imesikika tangu mapema asubuhi katika maeneo hayo ya mbuga ya wanyama ya Kahuzi-Biega. Emery Murhula ni mmoja wa wanaharakati wa asasi za kiraia katika wilaya ya Kabare, ambaye amethibitisha kwamba muda mfupi baadae, AFC/M23 walijielekeza sehemu hizo ili kurejesha utulivu.

Huko Kivu ya kaskazini,jana Jumapili watoto wawili walipoteza maisha na mwanamke moja kujeruhiwa vibaya wakati wa shambulizi la Wazalendo dhidi ya ngome za AFC/M23 katika kijiji cha Bukumbirwa wilayani walikale ambacho hadi sasa kinadhibitiwa na AFC/M23.

Mapambano yashuhudiwa na kwenye maeneo mengine

Mapambano mengine yameripotiwa katika wilaya ya Masisi ambapo mashuhuda wanasema Wazalendo walifanikiwa kuteka vijiji vya Kashanje na Nyampanika, si mbali na kijiji cha Mweso.

Kongo: Muafaka wa Doha na tafsiri kinzani kutoka pande mbili

Katika eneo la Kivu Kusini, wakati huu ambapo hali ya usalama ni tete pia katika vijiji vya wilaya za Shabunda, Mwenga na Fizi, baadhi ya wakazi wanajiuliza maswali mengi kusuhu kuendelea kwa machafuko licha ya mikataba. Héritier Zahinda ambaye ni mwanaharakati wa viguvugu la Kiraia linalochunguza vitendo vya bunge na serikali, DOHA, alipendekeza kwamba Wazalendo pia inabidi washirikishwe katika mchakato wa amani.

Mashirika ya kiraia Bukavu yaanzisha kampeni ya kuhamasisha mazungumzo

Ni katika muktadha huu ambapo mashirika ya kiraia mjini Bukavu yameanzisha kampeni ya kulazimisha pande zinazozozana Kongo kwenda kwenye meza ya mazungumzo jumuishi kwakutarajia amani ya kudumu. Imam Saleh Radjabu ni Kiongozi wa Kongamano la madini yakiislamu Kivu Kusini, anahisi kwamba amani ya kudumu haitatoka Marekani, Qatar au popote pale isipokuwa Kongo kwenyewe.

Jumamosi, Serikali ya Kongo na Muungano wa Mto Kongo (AFC/M23) walitia saini Mkataba wa Mfumo wa amani ya kina mashariki mwa Kongo huko mjini Doha, chini ya upatanishi wa Qatar. Pande zote mbili zimethibitisha kuheshimu Katiba ya Kongo, uadilifu wa eneo lote la Kongo na kuheshimu sheria za kimataifa za kibinadamu, kurejesha mamlaka ya serikali katika eneo lote la Kongo, hasa katika maeneo yaliyo chini ya udhibiti wa AFC/M23. Majadiliano yajayo yatahitaji kufafanua hatua, ratiba na taratibu za mpango huo, zikihusisha mamlaka za mitaa, kimila na kisheria.